Trump apiga ‘stop’ usambazaji dawa za malaria, Ukimwi kwa nchi maskini

Marekani. Rais wa Marekani, Donald Trump ameagiza kusitishwa usambazaji wa dawa za Ukimwi, malaria na kifua kikuu kwa nchi zinazopewa misaada na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID).

Agizo hilo limetolewa leo Januari 28, 2025 huku hatua hiyo ikilenga kupitia upya miradi mbalimbali ya misaada lakini imeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wataalamu wa afya na mashirika ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa duru za kimataifa, agizo hilo linatarajiwa kuathiri mamilioni ya watu wanaotegemea huduma za matibabu kupitia programu kama Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Mpango huo, ulioanzishwa mwaka 2003, umeokoa zaidi ya maisha ya watu milioni 25 barani Afrika.

Aidha, mashirika yanayotoa msaada, likiwamo la Chemonics, yamesema hatua hiyo itavuruga upatikanaji wa dawa na huduma kwa watu walioko hatarini zaidi.

Katika hatua nyingine, wataalamu wa afya wameonya kuwa, uamuzi huo unaweza kusababisha mlipuko mpya wa magonjwa, huku dawa zinazozuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa watoto milioni 6.5 katika nchi 23 zikiwa hatarini kutopatikana.

Hata hivyo, hatua hiyo pia inaweza kuchangia kuibuka kwa magonjwa sugu kutokana na upinzani wa dawa, jambo litakaloathiri juhudi za kimataifa za kukabiliana na magonjwa haya hatari.

Hatua ya Trump pia inajumuisha amri kwa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kusitisha ushirikiano wake na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Wataalamu wanasema uamuzi huu utaathiri mapambano dhidi ya tishio la magonjwa ya kimataifa kama homa ya ndege, virusi vya Marburg na mlipuko wa Mpox.

Mashirika ya misaada yameitaja hatua hiyo kuwa ni maangamizi ya moja kwa moja kwa watu wanaotegemea msaada wa kimataifa kutoka Marekani.

Related Posts