Meneja wa Mbowe aeleza mitihani ya Lissu Chadema

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uongozi mpya chini ya Tundu Lissu unakabiliwa na mambo matatu, ikiwemo kuvunja makundi na kukipeleka chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Mambo hayo yamebainishwa na Daniel Naftari, aliyekuwa Mratibu wa Kampeni za Freeman Mbowe, aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21 kabla ya kuchaguliwa Lissu kwenye mkutano wa Januari 21, 2025, uliofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Lissu, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, alishindana na Mbowe huku mvutano mkubwa ukiibuka baina ya makundi mawili. Kila upande ulituma mashambulizi ya hoja na kejeli dhidi ya wapinzani wao.

Hata hivyo, wajumbe 513, sawa na asilimia 51.5 ya wapiga kura 999, walimchagua Lissu kuwa mwenyekiti, huku Mbowe akipata kura 482 (asilimia 48.3). Charles Odero alipata kura moja, huku kura tatu zikiharibika.

Mbowe alikubali matokeo hayo na kumtakia heri Lissu, akimtaka kuunda kamati ya ukweli na upatanishi ili kutibu vidonda vilivyotokana na uchaguzi huo. Lissu alikubali hoja hiyo.

Leo, Januari 28, 2025, Naftari alitembelea ofisi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam, na kuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo mgombea wake (Mbowe) kukubali matokeo na kile ambacho Lissu anapaswa kufanya ili Chadema iendelee kusonga mbele.

Naftari amesema baada ya kushuhudia minyukano mikubwa iliyojitokeza kipindi cha kampeni za uchaguzi, jukumu la kumaliza tofauti limebaki upande wa walioshinda uchaguzi, ambao wanatakiwa kuunganisha chama ili kuwa wamoja.

“Kama mratibu wa kampeni ya Mbowe, tulishafanya tulichotakiwa kufanya. Tulizungumza na vyombo vya habari kuutakia kila la heri uongozi mpya. Maisha baada ya hapo yanashikiliwa na wenzetu walioshinda,” amesema.

Amesema matamanio yao ni upande ulioshinda waendeleze walipoishia, kutibu makovu, makundi, na minyukano iliyojitokeza.

“Tunashuhudia minyukano bado inaendelea na si jambo zuri, lakini ni mtihani unaotakiwa kubebwa na uongozi mpya. Lazima uishi hii falsafa ya ‘Strong Together’ ili kumaliza minyukano inayoendelea,” amesema.

Naftari amesema ushindi wa tofauti ya kura 31 dhidi ya Mbowe usiwape kiburi. “Ukishinda uchaguzi katika mazingira haya na mtu kama Mbowe mwenye wasifu mkubwa unapaswa kuwa makini, hasa katika kuunganisha chama ili kwenda mbele. Ukijisahau, hatuwezi kuwa wamoja,” amesema.

Amesema Mbowe, baada ya kuongoza chama hicho kwa miaka 21, bado ana nguvu ndani na nje ya chama, na hawezi kudharauliwa. “Ana watu wengi wanaomuamini kwa sababu ya utawala wake wa muda mrefu,” amesema.

“Ili minyukano hiyo iishe, ni lazima uongozi mpya uonyeshe uko tayari kumaliza minyukano. Na moja ya njia ya kumaliza ni kutokuendeleza makundi. Wapo wanaofahamika upande wa Mbowe, ikionekana wanabaguliwa, itakuwa si sahihi,” amesema.

Amesema jambo wanalopaswa kulifanya ni kama alivyoshauri Mbowe, kuundwa tume ya ukweli na upatanishi. “Malengo yetu ilikuwa kama tungeshinda, tulipanga kuunda tume hii haraka zaidi, hata kabla ya kuunda sekretarieti,” amesema.

Amesema uongozi wa Lissu kwa sasa ili afanikiwe anahitaji zaidi umoja, kwani waliowengi waligawanyika kupitia uchaguzi huo. “Mbowe alitangaza umoja wakati anatoka, sasa lazima usimamiwe kwa nia ya dhati na viongozi walioshinda,” amesema.

“Lissu anapaswa kujua kuiongoza Chadema hii hakuhitaji uwezo pekee yake, inahitaji hekima ya uongozi wa kuongoza watu wako na wasio kuwa wa kwako wakati wa kampeni busara hiyo namuombea awe nayo akifanikiwa kwenye mtihani huo atakuwa amefanikiwa,” amesema

Katika maelezo yake, Naftari amesema Chadema haiongozwi kwa mujibu wa katiba pekee yake, bali lazima kuangaliwe hali ya kisiasa. “Ukitafsiri katiba pekee yake unaweza kufukuza watu wengi. Hata Lissu mwenyewe angeweza kufukuzwa uanachama,” amesema.

Naftari amesema Lissu anafaa kuwa kiongozi, lakini kuna wakati amekuwa na uamuzi mgumu dhidi ya uamuzi fulani wa chama. “Si jambo baya, lakini lazima kuamini kwenye ushirikishwaji wa pamoja. Si kila wakati utatafsiri katiba ili kuongoza chama,” amesema.

“Mbowe katika kufanya uamuzi anatumia busara zaidi, hasa yanayohusu hatima ya chama, jambo ambalo Lissu hana. Lissu ni mtu wa uamuzi wa papo kwa papo. Hivyo ni watu wawili tofauti,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu misimamo ya Lissu, hususan msimamo wa chama cha ‘No Reform, no election’, Naftari amesema: “Huu ni mtihani wa kwanza wa Lissu, anaopaswa kushinda.”

Amesema Mbowe alikuwa akiamini kwenye maridhiano, kwamba maandalizi ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na wagombea, yanahitaji shinikizo la mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili kuruhusu uchaguzi huru na haki. “Mazingira ya kiuchaguzi ya nchi hii ni mabaya na sheria za uchaguzi ni mbovu, hazirekebishiki, zinahitajika kuandikwa upya,” alisema Lissu.

Akiendelea, Naftari amesema Chadema ni taasisi kubwa inayoundwa na maslahi ya mtu mmoja mmoja na maslahi ya pamoja ya kupigania demokrasia na maendeleo ya watu wote.

“Maslahi ya mtu mmoja mmoja ni mtu amejiunga na chama hiki ili apate udiwani, ubunge, na wengine urais. Ukisema chama hakishiriki uchaguzi, manake unagusa makundi mengi,” amesema.

Amesema ufafanuzi unahitajika kwa kuwakutanisha wanachama, na kuingia kwenye mjadala wa pamoja kuhusu jinsi ya kufika 2025 bila uchaguzi. “Katika kipindi ambacho Chadema inahitaji kuwa moja ili ifanikiwe, ni kwenye hii falsafa ya ‘no Reform no election’. Haipaswi kuwa msimamo wa kundi fulani, unapaswa kuwa msimamo wa wanachama wote,” amesema.

Amesema kauli ya kuunganisha wanachama inapaswa kutekelezwa kwa vitendo na si kwa maneno. “Kwa uzoefu wangu, si watu wote wanakubaliana na kauli ya kususia uchaguzi. Watu wanaweza kukubali kufanya maandamano, lakini si kukaa pembeni na kushuhudia vyama vingine vikishiriki uchaguzi,” amesema.

Amesema katika jambo hilo, Mbowe alikuwa anaamini kutumia njia zote za kisiasa, ndiyo maana walikuwa wanaamini maridhiano yalikuwa moja ya lengo la kufikia mabadiliko ya sheria.

“Tulikuwa tunaamini hivyo, lakini katika mazingira tuliyonayo, njia rahisi ya kufanikiwa kisiasa ni kushirikiana na Serikali,” amesema Naftari.

Related Posts