Marais wa Afrika wataja matumaini uzalishaji umeme

Dar es Salaam. Baadhi ya marais wa nchi za Afrika wanaohudhuria mkutano mkuu wa nishati Afrika, wameeleza matumaini yao kuhusu mkakati ulioandaliwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme barani humo.

Mkutano huo wenye kauli mbiu ya Ajenda 300, ulioanza kufanyika jijini Dar es Salaam tangu jana Januari 27 na leo Januari 28, umehudhuriwa na marais  21 wanaowakilisha mataifa ya Tanzania, Lesotho, Djibouti, Jamhuri ya Congo Brazzaville, Visiwa vya Comoro, Madagascar, Somalia, Sierra Liane na Mauritania.

Wengine ni kutoka Burundi, Guinea Bissau, Malawi, Libya, Zambia, Kenya, Nigeria, Gabon, Liberia, Ethiopia, Botswana na Ghana.

Marais hao pamoja na mengine wamepitisha Azimio la Dar es Salaam linalolenga kuongeza uzalishaji na uunganishaji wa umeme kwa watu milioni 300.

Akizungumza katika mjadala katika mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Congo Brazzaville, Dennis Sassou Ngueso amesema katika nchi yake wana matumaini na mradi wa umeme wa Bonde la Mto Congo utakaozalisha megawati 200,000.

“Katika nafasi yangu kama rais nasimamia mradi wa Bonde la Mto Congo. Bonde hilo limejaa fursa ya kiwango cha megawati 200,000.

“Pia kuna nishati ya jua ambayo ni kilowati 7.5 kwa kilometa za mraba moja. Ninaposema hivyo, ninafikiria miradi hii mikubwa katika Bonde la Congo,” amesema. 

Amesema mradi huo utakapokamilika umeme wake utanufaisha bara zima. “Ili kutekeleza mradi huu wa Mto Congo, megawati zitakazopatikana ni 200,000 zitazalishwa kwa ajili ya Afrika. Kwa hiyo napongeza shughuli ya leo ambayo ni kwa ajili ya Afrika.”

Mfalme Letsie III wa Lesotho amesema nchi hiyo imejizatiti kuongeza uzalishaji wa umeme kwa wananchi wake.

“Afrika ikiwamo Lesotho, imebarikiwa rasilimali na fursa nyingi, lakini bado zaidi ya watu 600 milioni hawana nishati na ni sehemu ya umasikini na inapunguza huduma za afya,” amesema.

Ameongeza kuwa changamoto hizo ndio zinaleta fursa ya kutafuta njia zaidi za kuzalisha umeme.

“Kwetu sisi Lesotho kuyafikia malengo haya ya Ajenda 300 tunalenga maeneo kadhaa ikiwamo kupanua nishati jadidifu.

“Tunajenga mazingira mwafaka katika nishati safi ambayo itakidhi mahitaji ya nyumbani na kuifanya Lesotho kuwa muuzaji wa nje ya mipaka ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) na nje ya hapo.”

Ametaja pia, mikakati ya usambazaji umeme ikiwa pamoja na kuunganisha makazi vijijini na kuvutia wawekezaji kutoka sekta binafsi.

Rais wa Umoja wa Visiwa vya Commoro, Azali Assoumani amesema nchi yake ina mpango wa kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa kutumia ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.

“Hivi karibuni tumezipitia sheria za uwekezaji ambao tunarahisisha uwekezaji kutoka sekta binafsi, hivyo tutakuwa na mifumo ya uwekezaji wa nishati safi na itakuwa ya bei nafuu kama zilivyo nchi nyingine,” amesema Assoumani.

Ametaja vyanzo vya umeme wanavyotarajia kuvitumia ni pamoja na joto ardhi na umeme jua, akisema vitakapoanza kutumika watafikisha asilimia 80 ya waliounganishwa na umeme.

Kwa upande wake Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimye amesema nchi yake inaendelea na utekelezaji wa miradi ya nishati.

“Sisi tuna mkakati wa ujenzi wa viwanda na uchimbaji wa madini, ujenzi wa shule na miundombinu ya usafirishaji na vyote vinalenga kuimarisha ustawi wa watu wetu,”amesema Ndayishimye.

Ametaja vyanzo wanavyotarajia kuvitumia kukuza uzalishaji kuwa ni mabwawa ya uzalishaji na umeme jua. 

“Tunaendelea kufanyia kazi miradi mingine itakayoipa Burundi megawati 27 za umeme na mwingine wa megawati 20 na kuna mradi pia wa megawati 49 ambao uko mbioni kukamilika.

“Katika usafirishaji wa umeme tunatarajia umeme kutoka Ethiopia na sasa uko kwenye mchakato wa kujenga nguzo, ambao tutapata megawati 200 na tunatarajia pia kununua umeme kutoka Tanzania utakaopita ushoroba wa kati,” amesema Ndayishimye.

Naye Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amesema tangu ameingia madarakani miaka minne iliyopita ameongeza idadi ya wananchi waliounganishwa na umeme kutoka asilimia 12 hadi asilimia 25.

“Hivyo Wamalawi wengi wamepata umeme kuliko wakati wowote wa historia tangu tupate uhuru na hapo ni mwanzo tu, tunatakiwa kuongeza kutoka asilimia 25 kufikia asilimia 70 kufikia 2030.

“Tunataka kufikia nyumba 2.7 milioni kwa kupitia gridi ya taifa na nje gridi. Lengo letu ni kuwafikia wananchi tupate na kuhakikisha kuna nishati ya kuaminika katika vituo vya shule, elimu na matibabu na kutengeneza ajira kufikia ya vijana,” amesema.

Amesema katika utawala wake anataka Malawi iungane na nchi zenye viwanda vingi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika, akishirikisha wadau hasa sekta binafsi.

“Kwetu Malawi tumeingia katika barabara ya kuhakikisha kuwa nishati inaweza kuwafikia watu wetu wote,” amesema Chakwera.

Related Posts