TASAC YAKABIDHI VIFAA TIBA SUMBAWANGA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 28 Januari, 2025, limekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milion kumi 10 katika vituo vitatu vya afya wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa ili kusaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa vifaa tiba katika vituo hivyo.

Msaada huo umetolewa kufuatia uhitaji wa vifaa hivyo mara baada ya kutokea kwa dhoruba ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa.

Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, Ofisa Mwandamizi wa TASAC, Naho. David Chiragi amesema lengo la msaada huo ni kuhakikisha wanapunguza upungufu wa vifaa tiba.

“Tumetoa msaada huu baada ya tukio la wavuvi 550 kukumbwa na adha ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa uliosababisha watu 10 kufa maji ambapo tisa waliopolewa na mmoja hakuweza kupatikana,” amesema Naho. Chiragi.

Aidha amesema kuwa moja ya jukumu la TASAC ni kusimamia masuala ya usalama ulinzi na kuzuia uchafuzi wa mazingira utokanao na shughuli za usafiri wa vyombo vya majini ambapo msaada huo umetolewa katika kituo cha afya Mtowisa, zahanati ya Nankanga na zahanati ya Milepa.

Ameongeza kuwa TASAC wanaishukuru Serikali kwa kuonesha umoja na mshikamano na kuhakikisha zoezi la uokoaji linafanikiwa kwa kuokoa wavuvi 540 waliokumbwa na adha hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Chirugile akipokea msaada huo wa vifaa tiba katika zahanati ya kijiji cha Nankanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliwashukuru TASAC pamoja na Wizara ya Uchukuzi kwa msaada huo muhimu kwa Bonde la Ziwa Rukwa ambao utapunguza adha kwa wagonjwa na akina mama wajawazito kutokana na upungufu wa vifaa tiba katika vituo vya afya.

Msimamizi wa kituo cha kata ya Nankanga Elladonna Mpumpa alishukuru TASAC na Serikali kwa ukombozi mkubwa ambapo amesema wamekuwa na upungufu wa vifaa tiba na wagonjwa wanaopumzishwa katika zahanati hiyo ni wengi na imekuwa ni changamoto hasa katika vitanda ambapo kwa msaada huo unakwenda kupunguza changamoto hiyo.

Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Nankanga wilaya ya Sumbawanga, Bw. Morice Fwaka kwa niaba ya wananchi aliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa msaada wa vifaa tiba ambapo msaada huo utakwenda kupunguza adha ya wagonjwa kulala wawili katika kitanda kimoja hasa akina mama wajawazito.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa  Nyakia Churugile akikabidhiwa wa kwa vituo vitatu vya afya kutokana na madhara ya  upepo Mkali katika Ziwa Rukwa kutoka kwa niaba niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, Ofisa Mwandamizi wa TASAC, Nah. David Chiragi.
 

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa Nyakia Chirungile akizungumza  wakati hafla ya kukabidhiwa vifaa vya vituo vitatu vya afya kutoka Shirika la Uwakala wa  Meli Tanzania (TASAC) kutokana vituo hivyo kuathiriwa na Upepo mkali wa Ziwa Rukwa.
 

Ofisa Mwandamizi wa TASAC, Nah. David Chiragi akizungumza  niaba niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum wakati wa kukabidhi vifaa mbalimbali katika Vituo Vitatu Afya vilivyoathuriwa na Upepo mkali  Ziwa Rukwa

 

Matukio  katika picha wakati wa Makabidhiano ya vifaa mbalimbali kwa vituo vitatu vya afya katika Wilaya ya Sumbawanga vilovyoathiriwa na upepo mkali wa Ziwa Rukwa.
 

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Chirugile (kulia) akipokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 kutoka kwa Ofisa Mwandamizi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Naho. David Chiragi (kushoto) ambaye alikabidhi msaada huo kwa niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum. Msaada huo umetolewa baada ya tukio la wavuvi 550 kukumbwa na adha ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa na kusababisha vifo vya watu 10.
 

Baadhi ya wakazi vitongoji vya Mtowisa, Nankanga na Milepa wakionesha baadhi ya vifaa tiba viliyotolewa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC). Msaada huo umetolewa baada ya tukio la wavuvi 550 kukumbwa na adha ya upepo mkali katika Ziwa Rukwa na kusababisha vifo vya watu 10.

Related Posts