Waziri Ndejembi atembelea OSHA, asisitiza uwekezaji zaidi katika TEHAMA

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),
Deogratius Ndejembi amefanya ziara katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya
Mahali pa Kazi (OSHA) jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujifunza jinsi Taasisi hiyo
iliyopo chini ya Wizara yake inavyotekeleza majukumu yake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi akizungumza na Viongozi wa Menejimenti ya OSHA wakati wa ziara yake ya kutembelea Ofisi za OSHA Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia mwenendo wa kiutendaji wa taasisi hiyo.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni takribani mwezi mmoja baada ya Kiongozi huyo kuteuliwa
na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo ya kusimamia Masuala ya Kazi
na Ajira nchini kutokana na mabadiliko madogo yaliyofanyika katika Baraza la Mawaziri
Machi 31, 2024.

Akizungumza na Menejimenti ya OSHA mara baada ya kusikiliza wasilisho la Mtendaji
Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, kuhusu OSHA na majukumu yake, Waziri
Ndejembi ameitaka menejimenti ya OSHA kuwekeza zaidi katika mifumo kidijitali ili
kurahisisha utendaji na kuongeza ufanisi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (kulia) na Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Comrade. Hery Mkunda (kushoto) wakisaini hati ya Makubaliano baina ya OSHA na TUGHE ya mashirikiano ya kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wafanyakazi nchini mbele ya Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, Deogratius Ndejembi.

Kadhalika, ameiagiza OSHA kuongeza jitihada katika kuwaelimisha na kuwahamasisha
wadau wa masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ili waweze kutekeleza sheria na
miongozo mbali mbali ya usalama na afya kwa hiari.

“Sina mambo mengi kwa siku ya leo kwani nimekuja kwa lengo la kujifunza kuhusu
utendaji wenu mkiwa miongoni mwa Taasisi chini ya Wizara ninayoiongoza ili kwa
pamoja tuweze kushirikiana kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu.

“Nimejifunza mengi kutokana na wasilisho la Mtendaji Mkuu hivyo ninawashauri
kuwekeza zaidi katika mifumo ya TEHAMA pamoja na kubuni mikakati ya kuongeza
uelewa miongoni mwa wadau wenu na wananchi kwa ujumla ambao uelewa wao
kuhusu masuala haya bado ni mdogo,” ameeleza Waziri Ndejembi.

Aidha, Ndejembi ameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Mashirikiano (Memorandum of
Understanding) baina ya OSHA na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya
Tanzania (TUGHE) yatakayoziwezesha Taasisi hizo mbili kushirikiana katika mambo
mbali mbali hususan suala la utoaji elimu ya usalama na afya kwa wanachama wa
TUGHE nchini.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, pamoja na
kuwasilisha mada kuhusu utendaji wa OSHA katika kikao hicho, amempongeza Waziri
Ndejembi kwa kuteuliwa kuiongoza Wizara ya Kazi na Ajira ambapo amemuahidi Waziri
kuhakikisha kwamba Taasisi ya OSHA inatekeleza wajibu wake ipasavyo.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kututembelea ambapo tumepata fursa ya
kumpitisha katika majukumu yetu nae ametushirikisha maono yake kuhusiana na sekta
hii ya Kazi na Ajira hususan eneo hili mtambuka la usalama na afya mahali pa kazi
ambalo linagusa kila sekta. Hivyo, tunamuahidi yeye (Mhe. Waziri) pamoja na Mheshimiwa Rais aliyemteua kuwa tutafanya kazi kwa bidii katika kufanikisha maono ya
viongozi wetu,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akiwasilisha mada juu ya mwenendo wa taasisi ya OSHA mbele ya Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi Pamoja na viongozi wa menejiment ya OSHA wakati wa kikao kifupi na Waziri huyo.

Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda, amesema makubaliano waliyofanya na
OSHA yanalenga kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapatiwa haki yao ya msingi ya
kulindwa kutokana na vihatarishi mbali mbali mahali pa kazi.

“Kwa mujibu wa Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambayo nchi yetu
imekubaliana nayo, masuala ya usalama na afya yamekuwa ni haki ya msingi ya
wafanyakazi hivyo sisi kama TUGHE tumeona ni muhimu tukafanya kazi kwa karibu na
OSHA ili kuhakikisha kwamba haki hiyo inapatikana,” ameeleza Comrade Mkunda.

Related Posts