Uchaguzi unapoisha, macho yote humtazama aliyeshinda. Matarajio huwa mengi endapo mshindi anakuwa mpya kwenye kiti. Mategemeo huwa na nguvu zaidi pale mshindi mpya anapofanikiwa kupitia agenda ya kumsiliba mtangulizi wake.
Ilitokea Kenya kama mfano dhahiri. Rais William Ruto, hadi sasa bado anateswa na urais wake. Tangu alipokula kiapo kuiongoza nchi hiyo, Septemba 13, 2022, amekuwa akikumbwa na misukosuko mingi. Kuanzia maandamano ya Raila Odinga hadi ya Kizazi Z (Gen Z).
Kikubwa kinachomtesa Ruto ni mguu alioingilia Ikulu Kenya. Alikuwa Naibu Rais, lakini akajitenga na changamoto za wakati wa uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, wakati yeye ndiye alikuwa msaidizi mkuu. Akahakikisha propaganda zinashika mpini. Akasema, hali ngumu ya maisha ya Wakenya ilisababishwa na mwafaka baina ya Uhuru na Raila.
Ruto alijenga ahadi kwa Wakenya bila uhalisia. Alisema, endapo angechaguliwa kuwa Rais wa Kenya, gharama za maisha zingeshuka na uchumi wa nchi ungejengwa kuanzia kwa watu wa chini kwenda juu. Baada ya kila tambo na propaganda anuwai, Ruto ndiye Rais sasa.
Wananchi wa Kenya hawaoni kile walichoahidiwa. Zaidi, wanaona maisha yamekuwa magumu kuliko nyakati za Uhuru. Si kwamba Ruto ndiye anasababisha maisha yawe magumu, bali mazingira ya nchi na mzunguko wa dunia. Hata hivyo, Wakenya hawana muda wa kumwelewa. Waliambiwa maisha yangekuwa nafuu na hayawi.
Ruto anateswa zaidi na mguu alioingilia. Ni ushuhuda jinsi karma inavyodai madeni yake. Inashabihiana na msemo “what comes around goes around”, kama alivyoandika Eddie Stone, katika kitabu chake kinachoitwa “Donald Writes No More”, ambacho ni chapisho la mwaka 1974.
Ruto kwa kuona ni turufu yenye nguvu kumpa urais, alithubutu kusema Uhuru na Raila, ndiyo sababu ya ugumu wa maisha. Raila hakuwa kiongozi serikalini, Ruto alijua hilo, lakini alifanya kampeni chafu. Alisema, yeye akiingia ofisini, kila kitu kingekuwa sawa.
Matokeo yake, Ruto amefanya mapatano na Raila. Tena, imemlazimu kumtosa aliyekuwa naibu wake, Rigathi Gachagua, na kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, kwa kuingiza watu wa Raila. Ruto alimkosoa Uhuru kwa kufanya maridhiano na Raila, lakini yeye ameunda serikali ya pamoja na timu ya Raila. Uswahilini huhoji “kiko wapi?”
Dk Benson Bagonza, Askofu Mkuu wa KKKT, Dayosisi ya Karagwe, baada ya Tundu Lissu kushinda uenyekiti Chadema dhidi ya mtangulizi wake, Freeman Mbowe, alisema kumwambia Lissu: “Mahaba ya kutongozea na kuolea ni tofauti na mahaba ya kuishi katika ndoa.”
Maneno haya ya Askofu Bagonza, yana maana kubwa sana. Kuanzia kwa Ruto hadi kwa Lissu. Upande wa Ruto alishayaona, kwamba mahaba ya kutongozea (maneno ya wakati wa kampeni), siyo utakayotumia ukiwa kwenye kiti.
Kama ambavyo Ruto hawezi kusema tena kuwa maridhiano ya Uhuru na Raila ndiyo yanasababisha ugumu wa maisha Kenya na ukosefu wa ajira, bali yeye ndiye anapaswa kuonesha ufumbuzi, ndivyo kwa Lissu. Baada ya maneno mengi kumkaanga Mbowe kuwa aliidumaza Chadema kwa maridhiano na Rais Samia Suluhu Hassan, sasa kazi kwake. Wakati Lissu alikuwa Makamu Mwenyekiti Chadema, mtu wa pili kimamlaka baada ya Mwenyekiti.
Utaona mitandaoni, vijana waliokuwa wanamuunga mkono Mbowe, sasa hivi wanaikejeli Chadema ya Lissu. Kwamba hawataki maridhiano, wanataka kuandamana. Lissu ana wiki moja tu tangu ameingia ofisini. Anajengewa mazingira kuwa ana mzigo mkubwa na mzito wa matarajio.
Timu ya Mbowe wanahoji, mbona Dk Willibrod Slaa yupo mahabusu bila dhamana na hakuna maandamano? Ni kwa sababu imani kubwa ilijengwa kwamba Chadema ya Mbowe ilipoa, ilikuwa legelege, ya Lissu ni ya moto, ukiweka kigingi cha mti, ataweka chuma.
Ni kwa sababu kila lawama ya anguko la Chadema, alitupiwa Mbowe. Uchaguzi ulioharibiwa wa serikali za mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020, hadi uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, Mbowe ndiye mbeba lawama, kwamba alikuwa legelege, na alilamba asali.
Sasa, subira haitakuwepo tena. Lissu anatakiwa kuonesha matokeo. Vitendo vya utekaji vikome na majibu ya waliopotea huko nyuma au waliouawa. Mwaka huu ni wa uchaguzi, agenda ya Chadema ni bila mabadiliko ya kikatiba na mifumo ya uchaguzi, hakuna uchaguzi (No Reforms, No Election).
Agenda hii, Lissu hapaswi tena kuitumia kushinda kiti cha uenyekiti, anatakiwa kuisimamia na kuongoza chama kuifanikisha. Macho yote yapo kwake. Amehama upande wa kulalamika, sasa yeye ndiye atabeba lawama kama aliyoyalalamikia, hayatakuwa na mabadiliko. Ni kama Ruto Kenya, ndivyo Lissu na Chadema.