Wadau wamlilia Bwire, wataja vilivyombeba

WAKATI maandalizi ya kuupumzisha mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza na Kulea vipaji cha Alliance, Jame Bwire yakiendelea kabla ya kuzikwa wikiendi hii, baadhi ya wadau wa michezo nchini wametaja mambo yaliyombeba kigogo huyo na kuacha alama kubwa ambayo haitafutika kirahisi.

Bwire ambaye alikuwa mdau mkubwa wa michezo nchini akiwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza na Kulea vipaji cha Alliance, aliwahi pia kuwa mwanasiasa akiwa Diwani wa Kata ya Mahina Jimbo la Nyamagana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, alifariki dunia Januari 25 jijini Mwanza.

Mwanamichezo huyo anayetarajiwa kuzikwa Jumapili hii mkoani Mara, alikuwa ni mmoja kati ya watu ambao wameweka alama ya kukumbukwa kwenye michezo Tanzania kutokana na kituo chake kuzalisha wachezaji wengi mahiri kwenye soka upande wa wanawake na wanaume wanaofanya vyema ndani na nje ya nchi.

Kifo chake kimewashtua wengi na baadhi yao wamezungumzia watakavyoendelea kumkumbuka kwa kutaja sifa kubwa alizokuwa nazo ni nidhamu, uthubutu wa kusimamia maono yake na upendo wa kusaidia watoto wa Kitanzania wapate elimu na kukuza vipaji vyao, ni kati ya silaha zilizombeba James Bwire na kutimiza mambo makubwa aliyoyafanya katika sekta ya michezo.

Licha ya msiba huo, Alliance Girls iliendelea na ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake kwa kucheza jana Jumanne dhidi ya Yanga Princess kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, huku Ofisa Habari wa timu hiyo, Simon Kabwema akisema baada ya mchezo huo walianza safari kurudi Mwanza ili kumuaga mkurugenzi huyo.

Mtoto wa marehemu, Nelson Marwa ambaye ni Katibu Msaidizi wa Alliance, alisema baba yake ambaye alikuwa ni muumini wa dhehebu la Kisabato, ataagwa na umma Ijumaa katika makazi yake Mahina jijini Mwanza.

Marwa alisema kinachoendelea kwa sasa ni utaratibu wa kawaida wa maombolezo nyumbani kwa Bwire (Mahina), ambapo Ijumaa ndipo mwili utatolewa mochwari kupelekwa nyumbani ili kuagwa na wadau na waombolezaji mbalimbali kabla ya kusafirishwa Jumamosi kwenda Tarime na kuzikwa Jumapili katika kijiji cha Nyamwaga.

“Wageni mbalimbali kutoka kada tofauti, ndugu na marafiki wanaendelea kufika nyumbani kutoa salamu za pole. Kwa aliye karibu anaweza kufika kushiriki hiyo Ijumaa na atakayewiwa zaidi anaweza kuungana nasi kwenda kumpumzisha mzee nyumbani Tarime,” alisema Marwa.

Akizungumzia mchango wa Bwire, kocha mkongwe, John Tegete alisema Bwire hawezi kusahaulika katika sekta ya michezo mkoani Mwanza kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya kwa kuinua wachezaji ambao wengine wanacheza barani Uyala ikiwa ni historia ambayo haifutiki.

Tegete aliyefanya kazi na Bwire akiinoa Alliance kati ya mwaka 2016 hadi 2019 alisema timu waliyoitengeneza imeacha vipaji vingi kwa manufaa ya taifa, huku akimsifu kuwa ni mtu aliyetulia kwenye kuendeleza timu zake.

“Hakupenda utani kwenye kazi yake alikuwa ni mtu ambaye ni mwelewa kwamba hili ni kosa la kiufundi au la kifiziki timu kutokuwa vizuri, na aliwapenda sana wachezaji na timu yake kwahiyo usifanye mchezo na timu yake,” alisema Tegete na kuongeza;

“Aliwahi kufukuza vijana ambao walikuwa hawataki kufuata taratibu za mpira wakati tuko kwenye mashindano nchini Uganda, alikuwa hataki mchezo, alitaka nidhamu ya hali ya juu kutokana na historia yake ya kufundisha chuo cha ualimu kwahiyo alipenda wachezaji wawe na nidhamu.”

Mshambuliaji wa zamani wa Alliance FC, Seleman Kibuta alisema kutokana na heshima yake Bwire alimuamini na kumkabidhi majukumu ya uangalizi wa timu inaposafiri kwenye mechi, huku akiamini mkurugenzi huyo amefariki akiwa na kiu yake ya kuirudisha timu hiyo Ligi Kuu.

“Tanzania tumepoteza mtu muhimu katika tasnia ya michezo tutamkumbuka sana hususan walioishi naye watamkumbuka kwa ukarimu wake. Alinipa motisha nikiwa mchezaji mwandamizi katika timu yake ili kuwaongoza wenzangu na kituo chake,” alisema Kibuta na kuongeza;

“Alipenda kuniita ‘Mbuta’ kwa namna nilivyokuwa nikiongea naye au kuzungumza na wachezaji wenzangu, ilifikia hatua hadi timu ikitaka kusafiri ananiambia nakukabidhi timu najua kuna walimu na viongozi lakini wewe nakukabidhi timu nenda nayo naamini iko katika mikono salama.”

“Wakati huo sikuwa nahodha au kiongozi yeyote lakini alinipa wadhifa mkubwa kama vile rais wa timu kumwakilisha yeye. Nilikuwa nafarijika sana wakati ule anaponikabidhi timu nilikuwa naona ni bora niipambanie timu kwa sababu iko katika mikono yangu,” alisema Kibuta.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka la Wanawake Mkoa wa Mwanza, Sophia Makilagi alisema msiba wa Mkurugenzi huyo ni pigo kubwa kwa soka la wanawake mkoani humo kutokana na mchango mkubwa alioutoa ikiwamo kuanzisha timu ya Alliance Girls ambayo haijawahi kushuka tangu ipande Ligi Kuu mwaka 2017.

“Nimefanya naye kazi tangu nikiwa mwakilishi wa soka la wanawake mkoa wa Mwanza mpaka kuwa mwenyekiti wa chama mkoa, imeniumiza sana kwa sababu tumepoteza mwanamichezo na mtu ambaye ni mpambanaji hususan jinsi alivyotupambania soka la wanawake mkoani kwetu, hili tumelipokea kwa huzuni kubwa sana,” alisema Makilagi.

Kocha wa Ceassia Queens, Ezekiel Chobanka ambaye alidumu Alliance Girls kwa takribani miaka 10 tangu 2017 ilipoanzishwa na kupanda Ligi Kuu ya Wanawake, alisema matunda ya mradi waliouanzisha na Bwire kwenye soka la wanawake yamekuwa msaada mkubwa kwa taifa mpaka sasa.

Alisema walifahamiana na Bwire kwa mara ya kwanza mwaka 2017 wakati akiinoa Mvuvumwa FC iliyokuwa daraja la kwanza (sasa Championship) kwenye mchezo dhidi ya Alliance FC ambao walipoteza kwa bao 1-0 lakini Bwire akakoshwa na kiwango cha wapinzani wake na kumtafuta kocha huyo.

“Bwire alimtuma Jackson Mwafulango (aliyekuwa ofisa habari) achukue namba yangu tukaanza kuwasiliana akaniambia amefurahishwa na aina ya soka ambalo timu yangu inacheza na ndiyo falsafa ya timu za Alliance, hivyo, angependa nikafanye kazi naye, nilimkubalia na safari yetu ikaanzia hapo,” alisema Chobanka.

Aliongeza; “Ni mtu aliyekuwa na ushauri mzuri akikaa anakwambia mwalimu unaonaje au wewe una mtazamo upi, kwahiyo wewe unampa mtazamo anakuunga mkono anasema hili tulisukume nitakusaidia kwa asilimia 100 tutafanikiwa. Ukikaa siku mbili mpaka tatu anakuita anakuuliza yale mawazo tumefikia wapi.”

“Alikuwa ni kama mzazi ambaye anawajenga watu kuwa viongozi, ukiwa ni mtu ambaye hujawa imara kwenye kusimamia anakujenga unakuwa kiongozi namna anavyokupa msimamo, njia za uongozi na kukuelekeza. Ni mtu wa michezo na mtu wa watu,” alisema Chobanka aliyeondoka msimu huu kujiunga na Ceassia Queens ya Iringa.

Alisema kifo cha muasisi huyo wa Alliance ni pigo kubwa kwa taasisi na taifa kwa ujumla, huku akitoa wito kumuenzi kwa kile alichokianzisha ili kuyaendeleza maono yake ambayo mengine yalikuwa hayajatimia, ikiwa ni njia mojawapo ya kukumbuka mchango wake kwa taifa.

Related Posts