Masharti magumu mabosi Yanga, Ramovic hakuna namna

NDANI ya Yanga ni sawa na kile kidonda ambacho kinaonekana kimepona nje lakini ndani bado kuna shida. Baada ya timu hiyo kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua hiyo imewavuruga viongozi wao na hata mashabiki wao.

Yanga iliishia hatua ya makundi ikishindwa kumaliza kwa ushindi uliokuwa unahitajika ili itinge robo fainali kwa mara ya pili mfululizo.

Wanaweza kulaumiwa wote lakini kuna presha ya ndani ipo kwa kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic ambaye alishindwa kuiongoza Yanga kufuzu robo fainali licha ya kwamba hajawa na timu kwa muda mrefu kwani alitambulishwa Novemba 15, 2024 akichukua nafasi ya Miguel Gamondi.

Chanzo kutoka ndani ya Yanga, kinabainisha, Kocha Ramovic ana mambo mawili ya kufanya kuhakikisha analinda kiba-rua chake licha ya falsafa yake ya gusa achia twende kwao kukubalika vizuri.

“Kila mmoja alitarajia kuona Yanga ikifuzu robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mechi ya mwisho ikatoa matokeo mabaya zaidi kwetu kitu ambacho viongozi wameonekana kutokubaliana nacho,” kilisema chanzo hicho na kuongeza.

“Sasa basi kutokana na hilo, kocha ametakiwa kuhakikisha timu inatetea mataji yake mawili ya ndani kwa maana ya Ligi Kuu na Kombe la FA, lakini jambo lingine kushinda mechi kubwa kwa kuzifunga Simba na Azam tukikutana mzunguko wa pili.”

Yanga kama ingeshindwa kufuzu huku pia watani wao Simba wangekuwa kwenye anguko upepo ungeweza kutulia, lakini hatua ya Simba kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ndani ya Yanga hiyo inakuwa kama gesi inayo-karibia kulipuka kwa maana ukipita moto wowote hata mdogo unaweza kuamsha zogo jipya.

Pia Simba ndio wanaongoza msimamo wa ligi chini yake ipo Yanga, timu hizo mbili zikitofautiana pointi moja pekee. Mashabiki wa Yanga na hata viongozi wao wanaamini timu yao inaweza kurudi juu ya msimamo.

Yanga kuendelea kukaa chini ya Simba haiwafurahishi kabisa viongozi na mashabiki wa timu hiyo bila kujali ubora wa watani wao, hakuna ambacho utawaambia Yanga wekundu hao ni bora kushinda kikosi chao.

Ramovic ametakiwa kurudisha imani ya kwanza kwa kuipandisha Yanga juu ya msimamo lakini isitokee kinyume chake kwa kikosi chake kuendelea kuangusha pointi au kuoneakana hataweza kuwashusha wekundu hao.

Ubingwa Ligi Kuu Bara, FA

Yanga wanaweza kuvumilia kuishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini sio kushindwa kutetea mataji yao.

Ramovic ameanza vizuri safari ya kutetea Kombe la FA akishinda wikiendi iliyopita kwa mabao 5-0 dhidi ya Copco huku kwenye ligi wikiendi hii akiwa na nafasi ya kurejea kileleni kwa muda atakapoikaribisha Kagera Sugar kabla ya kesho yake Simba kucheza ugenini dhidi ya Tabora United.

Ukiwauliza mashabiki wa Yanga kuna kitu gani kitabaki kwenye mioyo yao juu ya kocha aliyeondoka Miguel Gamondi, jibu la haraka watakwambia Muargentina huyo aliwaheshimisha mbele ya watani wao Simba.

Gamondi ndio kocha ambaye hajawahi kufungwa na Simba ndani ya dakika 90 akipoteza mara moja tu tena mechi yake ya kwanza kwa matuta pale Tanga katika Ngao ya Jamii msimu wa 2023-2024, baada ya hapo Wekundu hao walipigwa kila walipokutana na Wananchi.

Mbali na rekodi hiyo, Gamondi ndiye kocha aliyewaheshimisha Yanga kwa kulipa kisasi cha mabao matano aliposhinda 5-1 msimu uliopita dhidi ya Simba.

Kama Ramovic akikutana na Wekundu hao kisha akapoteza hataweza kueleweka kirahisi kwa wafuasi wa timu hiyo wa-taona ni rasmi kocha huyo sio wa kiwango chao.

Msimu huu, mchezo wa mzunguko wa kwanza kwenye ligi Yanga ikiwa chini ya Gamondi, ilishinda 1-0, kabla ya hapo ilishinda 1-0 katika Ngao ya Jamii.

Mbali na Simba, kuna Azam ambao ndio walioanza kumtibulia Gamondi msimu huu kwani mchezo wa ligi mzunguko wa kwanza Yanga ilifungwa 1-0. Yanga nayo iliichapa Azam 4-1 katika fainali ya Ngao ya Jamii msimu huu, hivyo mchezo wa mzunguko wa pili umekaa kimtego.

Akizungumzia kibarua alichonacho mbele yake, Kocha Ramovic alisema anauona ugumu wa kushinda mataji ya ligi na Kombe la FA kutokana na presha iliyopo, pia ushindani kutoka kwa timu pinzani.

“Kushinda michuano hii (Kombe la FA) ni ngumu, tunajaribu kuwa bora, tunataka kupata ushindi kila wakati. Ni ngumu kwa sababu kuna timu nyingi za ushindani lakini tuna muda wa kujiandaa kujiweka sehemu salama,” alisema kocha huyo na kuongeza.

“Tunastahili kila mwaka kushinda ligi, hiyo ndiyo akili yetu na akili ya klabu kubwa kama hii.

“Hii ndiyo presha tuliyonayo, lakini ni kawaida kuwepo kwa klabu kama hii, tunataka kushinda ligi na FA, hayo ndiyo malengo yetu, vinginevyo halitakuwa jambo zuri.”

Related Posts