Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ) ameongoza mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa asasi hiyo.
Mkutano huo ulifanyika jana Januari 28, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam, huku mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) vya FARDC dhidi ya waasi wa M23 yakitajwa kuwa sababu ya mkutano huo.
Mkutano huo ulioongozwa na Rais Samia, ulihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Zambia, Hakainde Hichilema na Rais wa Jamhuri ya Malawi Dk Lazarus Chakwera.
Pia, ulihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Antoine Tshisekedi ambao walishiriki kwa njia ya mtandao.
Hali ya kiusalama imeendelea kuzorota nchini DRC kufuatia mapigano ya FARDC dhidi ya waasi wa M23 ambao wametangaza kuiteka miji ya mashariki mwa nchi hiyo ikiwemo Goma.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti leo Jumatano Januari 29, 2025, kuwa M23, mbali na kuiteka Goma, pia wamechukua udhibiti wa Uwanja wa ndege wa Goma.
Mapigano hayo jana yalisababisha kuibuka kwa maandamano yaliyosababisha uharibifu na uvamizi wa balozi za nchi mbalimbali jijini Kinshasa ikiwamo ubalozi wa Marekani, Ubelgiji, Kenya na Uganda.
Waandamanaji hao pia walichoma ubalozi wa Ufaransa na Rwanda huku uvamizi wa M23 ukitajwa kuwa chanzo cha machafuko yaliyosababisha kuvamiwa kwa balozi hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot alithinitisha ubalozi wao nchini DRC kwa kuandika kwenye akaunti yake ya kuwa: “Ubalozi wetu uliopo jijini Kinshasa umeshambuliwa kwa kuchomwa moto. Hata hivyo moto huo umeshadhibitiwa.”
Akizungumza kupitia televisheni ya Taifa hilo, Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya aliwataka waandamanaji kuachana na uamuzi wao wa kushambulia balozi hizo badala yake wadai haki yao kwa njia ya amani.
“Tuna kila haki ya kuonyesha hasira zetu ila naomba basi tueleze hisia zetu kwa njia ya amani. Naomba tusishambulie miundombinu ya balozi za wenzetu,” amesema Muyaya.
Shirika la Reuters pia limeripoti kuwa mapigano hayo yamesabisha vifo vya watu zaidi ya 25 huku 367 wakijeruhiwa kutokana na majibizano ya risasi mjini Goma.
Kuutwaa Mji wa Goma ni pigo kwa Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kufuatia mapigano yaliyodumu kwa miezi kadhaa kati ya M23 na askari wa Jeshi la nchi hiyo FARDC, huku Mji wa Goma ukiwa kitovu cha biashara katika Miji iliyopo mashariki mwa DRC.
Waziri wa Maendeleo ya Vijijini wa DRC, Muhindo Nzangi alithinitisha jana kuwa M23 wameshauteka Mji wa Goma kwa asilimia zaidi ya 80, huku akidai kuwa vikosi vya Jeshi la Rwanda vimeweka kambi katika maeneo mengine ya mji huo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.