Wadau wataka utafiti zao la mwani

Unguja. Wadau wa zao la mwani kisiwani hapa wameziomba taasisi za mwani kufanya tafiti ya kilimo hicho ili kujua madini yaliyomo kwa lengo la kupata uhakika wa kitaalamu unaothibitisha ubora wa thamani ya zao hilo.

Pia, wameiomba Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwawekea miundombinu ya kuvunia, kukaushia na sehemu ya kuhifadhia mwani ili kufanya mwani kuthaminika.

Akizungumza katika mkutano wa kuimarisha kilimo cha mwani kisiwani hapa leo Januari 29, 2025, mdau wa kilimo hicho, Asha Mussa amesema utafiti wa zao hilo utaleta ahueni kwao kwani itawasaidia kuongeza bei ya  mwani na kupata soko la uhakika. 

“Tunaziomba taasisi kufanya tafiti ya kilimo cha mwani kupata uhakika wa kujua madini yaliyomo katika zao hilo  kuwe na uhakika wa kitaalamu utaothibitisha ubora na thamani ya zao hilo na kuongeza bei nzuri na kupata soko la uhakika,” amesema Asha.

Ofisa Mkuu wa Tasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari, Ali Said amesema Serikali kupitia taasisi hiyo inaendelea kufanya utafiti wa mbegu za mwani kwa ajili ya kuimarisha ukulima huo na uzalishaji wa zao nchini.

“Uzalishaji kilimo cha mwani umekuwa kwa kiasi kikubwa kuliko uzalishaji wa mazao mengine kutokana na uwelewa mkubwa walionao wakulima wa mwani hivyo ni wakati sahihi wa kufanya tafiti juu ya kilimo hicho,” amesema Ali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi ukuaji viumbe maji baharini, Dk Hamis Nikuli amesema kupitia kikao hicho italazimika kwa washiriki kutoka na majibu mazuri ya zao la mwani ambayo yataleta tija zaidi kwa jamii.

“Kupitia kikao hiki tutatoka na maamuzi ambayo yatapelekea watunga sera kusaidia namna ya kupambana na changamoto ya zao la mwani,” amesema Hamis. 

Pia, amesema ipo haja kwa wataalamu kuendelea kutoa elimu ya ukulima wa mwani kwani unaweza kutengeza chakula cha mifigo hivyo upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa bei ya zao hilo.

Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwani (Zasco), Dk Masoud Rashid Masoud ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kununua mwani kwa wakulima kwa ajili kupeleka kiwandani ili kuwa na soko la uhakika nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Hamad Bakari Hamad amesema ushirikiano wa pamoja unahitajika kati ya Mashirika ya Maendeleo na Serikali ili kuhakikisha wakulima wa mwani wanapiga hatua ambayo italeta mabadiliko ya kuinua uchumi huo.

Wakati wa kubadilisha mazingira ya ukuzaji wa mwani kiuchumi umefika kwani zao hilo limepata nafasi ya kuwa zao kuu Zanzibar na kutambulika kimataifa,” amesema Hamad. 

Related Posts