Vituo vya afya vya kimkakati kuanza kujengwa kila jimbo

Dodoma. Serikali imesema mwaka 2025, itapeleka Sh250 milioni kwa kila jimbo kwa ajili ya kuanza kujenga vituo vya afya vya kimkakati Tanzania Bara.

Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba, amesema hayo leo Jumatano, Januari 28, 2025, wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Patrick Ndekademi.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itajenga kituo cha mkakati cha afya katika kata ya Old Moshi Mashariki.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema kuwa mwaka huu, Serikali italeta Sh250 milioni kwa ajili ya kuanza vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo yote Tanzania Bara, ikiwemo katika kata ya Old Moshi Mashariki.

Katika swali la msingi, mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu, amehoji lini Serikali itatenga fedha za kujenga vituo vya afya Kata za Misughaa, Issuna, na Mang’onyi.

Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali inatambua uwepo wa kata ambazo hazina vituo vya afya kote nchini, ikiwemo Kata za Issuna, Misughaa, na Mang’onyi katika Jimbo la Singida Mashariki.

Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka Sh1 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vya Ntuntu na Iglanson katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Ikungi itatenga Sh100 milioni kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Issuna, na Kata za Misughaa na Mang’onyi zitajengewa vituo vya afya kwa awamu kwa kuzingatia mahitaji na vigezo vilivyoainishwa.

Related Posts