Mbunge ataka sheria ya kuwahasi wabakaji watoto

Dodoma. Kwa mara nyingine suala la ubakaji bungeni, safari hii mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Asya Sharif Omar, amehoji ni lini Serikali itapeleka seria ya kuwahasi wabakaji wanaofanya udhalilishaji wa kijinsia kwa watoto.

Takwimu za Msingi Tanzania zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), zinaonyesha kuwa matukio ya ubakaji yameongezeka kutoka 8,691 mwaka 2022 hadi kufikia 6,827 mwaka 2023.

Mbunge huyo amehoji suala hilo bungeni leo Jumatano, Januari 29, 2025, na kujibiwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sajini.

Akijibu swali hilo, Sajini amesema Kifungu cha 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, imeainisha adhabu ya makosa ya kubaka kuwa ni kifungo kisichopungua miaka 30, viboko, na Mahakama inaweza kutoa amri ya kumlipa fidia muathirika wa tukio.

Aidha, amesema kifungu 131(3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kimeainisha kuwa ikiwa muathirika wa tukio ni mtoto mwenye umri chini ya miaka 10, adhabu pekee ni kifungo cha maisha jela.

“Serikali inalichukua swali la mheshimiwa mbunge kama sehemu ya maeneo ya kufanyiwa kazi na kuona kama ipo haja ya kuongeza adhabu kwa wanaobaka watoto chini ya miaka 10 au tuendelee na adhabu iliyopo ya kifungo cha maisha jela,” amesema.

Katika swali la nyongeza, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Ali Mzee, amehoji Serikali ina kauli gani kwa wazazi wanaomaliza kesi hizo mitaani badala ya kupeleka katika vyombo vya sheria.

Akijibu swali hilo, Sajini amesema makosa yote ya jinai yanapaswa kuripotiwa katika vyombo vya dola ili yafikishwe mahakamani.

“Sasa kama kuna watu wanaoyamaliza mitaani kupitia jukwa lako hili tuwasihi tusifumbie macho makosa makubwa kama haya ya ubakaji na udhalilishaji, inapotokea, turipoti polisi ili wafikishe mahakamani na stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria zilizopo,” amesema.

Related Posts