Serikali kukamilisha mwongozo wa watumishi wanaojitolea

Dodoma. Serikali imesema iko katika hatua za mwisho kukamilisha mwongozo utakaoangalia jinsi ya kuwaingiza katika mfumo watumishi wanaojitolea nchini.

Akizungumza bungeni leo, Jumatano, Januari 29, 2025, Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu alisema mwongozo huo utakuwa na mchakato wa kuwaingiza watumishi hao katika mfumo rasmi, baada ya maswali ya wabunge kuhusu stahiki zao. Alikuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Lulindi (CCM), Issa Mchungahela.

Katika swali lake, Mchungahela amehoji Serikali inazungumziaje watumishi wanaojitolea katika kada mbalimbali hususan kada ya elimu ambako kuna watu waliojitolea kwa zaidi ya miaka 10.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema jambo hilo limekuwa likizungumzwa mara kwa mara bungeni na kwamba Serikali iliahidi italifanyia mchakato ambao hivi sasa umefika katika hatua za mwisho.

Amesema wataomba ruhusa ya Spika wa Bunge, kushirikiana na kamati ya Bunge ili kuboresha jambo hilo vizuri na baadaye watatoa mwongozo katika mwaka huu huu wa fedha wa namna ambavyo watawaingiza kwenye mfumo vijana wanaojitolea.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mwantumu Zodo amesema kuna watumishi ambao wamestaafu tangu mwaka 2020, lakini hawajapata mafao yao na pia waajiri hawajapeleka fedha katika mifuko ya hifadhi ya jamii.

“Je Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa watumishi hao wanapata mafao yao?” amehoji Mwantumu.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema ni kweli kumekuwa na ucheleweshaji wa mafao kwa baadhi ya wastaafu unaotokana na baadhi ya waajiri kuwa wazembe kupeleka taarifa zao katika ofisi yake, ili wafanyiwe mchakato wa malipo kwa wakati.

“Nitumie Bunge lako kuwataka waajiri wote wastaafu wanapomaliza muda wao kufikisha taarifa zao kwa wakati ili ofisi ya Rais Utumishi ishughulikie jambo hilo kwa wakati na kama kuna wengine watabainika.

“Tulipitisha sheria hapa ndani ya Bunge, tutawachukulia hatua kwa sababu hatutaki kuona wastaafu wananyanyasika wakati wamefanya kazi yao ya kulitumikia Taifa kwa uadilifu,” amesema.

Amesema jambo la kustaafu halina udharura bali linafahamika, hivyo waajiri wanatakiwa kutimiza wajibu wao.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Janejelly Ntate amehoji Serikali imejipangaje kukwamua watumishi walioathiriwa na mwongozo wa upandaji madaraja wa miaka minne.

Akijibu swali hilo, Sangu amesema Serikali imekua ikifanya jitihada mbalimbali za kuoanisha na kuwianisha upandaji vyeo wa watumishi na katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imewapandisha vyeo watumishi 180,000 wakiwemo watumishi walioathirika na zoezi hilo.

Aidha, Sangu amesema katika utekelezaji wa Ikama na bajeti ya mwaka 2023/2024, Serikali imewapandisha vyeo watumishi 232,530 wakiwemo walioathirika na zoezi hilo, uhakiki wa vyeti feki na watumishi hewa.

Related Posts