Dar es Salaam. Wakati viongozi wa wa juu wa Chadema wakipanga wiki moja ya kikao cha kupanga mikakati ya kuendesha chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amesema chama hicho kitaendesha siasa za kushurutisha mageuzi ya kisiasa.
Lissu amesema hayo leo Jumatano, Januari 29, 2025, alipofika ofisi za makao makuu ya chama hicho Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa wiki moja iliyopita. Lissu amesema chama hicho hakitafanya siasa za kawaida.
Viongozi wengine waliokuwepo ni pamoja na Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche; Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Mzee; Katibu Mkuu, John Mnyika; na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa.
“Mimi ninaamini na nina ushahidi wa kutosha wa chaguzi tatu zilizopita zinaunga mkono kauli ya ‘No reforms, no election’ (hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi).
“Tukisema hivyo tunazungumzia njia zisizo za kawaida za kufanya siasa, njia za kushurutisha mageuzi, njia kawaida ni kwenda kuwaomba walete mageuzi,” amesema Lissu na kuongeza:
“Tunazungumzia njia za shuruti, ndivyo walivyofanya Kenya, Malawi, Zambia,” amesema Lissu alipoulizwa swali kuhusu kauli mbiu hiyo.
Alieleza kuwa chama hicho kinazungumzia njia zisizo za kawaida za kufanya siasa, njia za kushurutisha mageuzi. “Njia za kushurutisha, ndivyo walivyofanya Kenya, Malawi, Zambia.”
Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama muda wa kufanya mabadiliko hayo kupitia Bunge unatosha amesema, “Bunge linaweza kuitwa wakati wowote.”
“Hamjui historia ya nchi hii? Bunge liliwahi kukutana Jumamosi Aprili 25, 1964 wabunge wakaitwa walikokuwa wakaambiwa mkataba huu hapa, wakapitisha na Muungano,” amesema.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Bunge linaweza kuitishwa wakati wowote.
Akieleza sababu ya kufanya siasa za shuruti, Lissu amesema katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 2019, asilimia 36 ya wagombea wa Chadema walienguliwa na hata uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 pia hakuwa wa haki.
“Kwa hiyo tukisema twende na wao wanajua na Mungu anajua tunakwenda kuumizwa…tutakuwa sawa na makondoo yanayokwenda kuchinjwa.”
Huku akirejea maneno ya makamu wake, Heche, Lissu amesema katika utendaji wao hawatanyamaza hata wapelekwe gerezani.
“Utanyamaza ukiwa umekufa, ukiwa gerezani huwezi kunyamaza. Tukifanya harakati sawa sawa na tukifanya shuruti sawa sawa tutakwenda kuleta mageuzi kwenye uchaguzi,” amesema.
Akifafanua zaidi kuhusu kauli ya ‘No reforms, no election’, Lissu amesema hawamaanishi watasusia uchaguzi.
“Sio kwamba tutasusia uchaguzi, sio boycotting (gomea). Lazima tuzugumze hayo mambo mawili, tuone tutakwenda na yote kwa pamoja au moja,” amesema Lissu huku akisistiza kuwa hilo litategemea uamuzi wa vikao.
“Tunakwenda kujifungia, haitakuwa ya mwenyekiti, tutakuwa na retreat (tafakuri), tutajifungia.
“Tutazungumza lugha anayoweza kuielewa Samia (Rais Samia Suluhu Hassan). Nani anataka uchaguzi kama wa mwaka uliopita au wa 2020?” amehoji.
Akizungumzia mwelekeo wa siasa za chama hicho, Makamu Mwenyekiti (Bara), Heche amesema kuna mambo mengi ya kufanya kuleta mabadiliko na kuiondoa CCM madarakani.
“Sisi tutaongoza wananchi kuwakumbusha na kuwaondoa madarakani,” amesema.