Wagoma kubeba mimba, kisa kukosa huduma ya zahanati

  • Wanawake hao wamesema wanatumia nauli ya Sh14,000 mpaka Sh18,000  kutafuta huduma za afya Kijiji cha Bushiri

TS; Wakazi wa Kijiji cha Mwembeni hali hiyo inawaweka katika hatari ya kupoteza maisha wao au watoto watakaowazaa

S: Wanawake hao wamesema wanatumia nauli ya Sh14,000 mpaka Sh18,000  kutafuta huduma za afya Kijiji cha Bushiri

By Rajabu Athumani, Mwananchi

Pangani.  Baadhi ya wanawake wa Kijiji cha Mwembeni, Wilaya ya Pangani wanasema hawatabeba mimba kwa sababu eneo lao halina huduma za afya.

Wanasema hali hiyo inawaweka katika hatari ya kupoteza maisha wao au watoto watakaowazaa.

Wakizungumza kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdulrahman ya kukagua miundombinu ya afya na kuzungumza na wananchi  leo Jumanne Mei 14, 2024 wilayani hapa, wanawake hao wamesema wanatumia nauli ya Sh14,000 mpaka Sh18,000  kutafuta huduma za afya Kijiji cha Bushiri.

Anastazia Mulula, mkazi wa Kijiji cha Mwembeni amesema yeye mpaka sasa ana mtoto mmoja na sababu inayofanya achelewe kubeba ujauzito mwingine anahofia maisha yake kwa sababu zahanati ya jirani ni mbali na hapo wanapoishi.

Anastazia  amesema mtoto wake wa kwanza anasoma  kidato cha pili, hivyo anafikiria kama atabeba mimba nyingine sasa, hana uhakika wa kujifungua salama.

Aidha, Luciana Deus amesema alishuhudia mwanamke mwenzake mtoto akifia tumboni wakati akisafirishwa na pikipiki kupelekwa  zahanati ya jirani kujifungua.

Amesema kitendo kile kimewafanya wanawake wengi kijijini hapo kuwagomea waume zao kubeba ujauzito.

“Sisi tumeweka mkazo kweli, kwa kusema kuzaa hapana  kutokana na changamoto ya kukosa zahanati, kuna dada mmoja alikosa mtoto kutoka Kijiji cha Mwembeni kwenda Boza, kufika kule mtoto amefia tumboni kwa hiyo sisi tunachoomba ni kupata zahanati,” amesema Luciana.

Mmoja wa wanaume wa Kijiji cha Mwembeni, Juma Baruti amekiri kuwa wake zao wanawagomea kubeba ujauzito kwa sababu ya kukosekana kwa huduma ya wajawazito kijijini hapo.

Amesema hata wanaojitutumua kubeba ujauzito wanaishi kwa shaka kama watajifungua salama au la.

Ameongeza kuwa kutoka kijijini hapo kwenda Zahanati ya Boza wanasafiri kilomita saba mpaka nane, na gharama ya usafiri ni kubwa.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwembeni, Salim Ali amesema tayari wameshaanza ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho na mpaka sasa zaidi ya Sh28 milioni zimepatikana ikiwemo michango ya wananchi.

Amesema tayari wameshatandika jamvi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho, hivyo wanasubiri zege likauke waanze kujenga boma.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Abdulrahman amewatoa wasi wasi akiwaambia changamoto hiyo itamalizwa hivi karibuni.

Amechangia Sh10 milioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo huku akiwaomba wadau wengine nao wajitokeze kuchangia ujenzi huo.

Related Posts