Waliopewa uraia Singida BS kujua hatma yao kesho, TFF wafunguka

HATMA ya nyota watatu wa Singida Black Stars wanaodaiwa kubadili uraia ili kuwa Watanzania Josephat Arthur Bada, Emmanuel Keyekeh na Mohammed Domaro Camara inatarajiwa kufahamika baada ya kikao cha Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayokutana kesho kusikiliza mashauri mbalimbali likiwamo la wachezaji hao.

Wachezaji hao wamekuwa gumzo kwa karibu wiki nzima tangu ilipotolewa taarifa kwamba wamebadilisha uraia kutoka ule waliokuwa nao, huku kukiwa na sintofahamu kutokana na kudaiwa baadhi ya taratibu za kuwapa wageni uraia wa tajnisi kuonekana kama zimekiukwa.

Bada alitua nchini kama mchezaji wa kigeni akiwa ni raia wa Ivory Coast msimu huu akitokea Asec Mimosas, huku Keyekeh aliyetokea  Samartex ya kwao Ghana na Camara aliyejiunga pia na timu hiyo msimu huu akitokea Hafia ya Guinea, ambao kwa pamoja inaelezwa waliamua kuchukua uamuzi huo, huku viongozi wa kikosi hicho wakibariki na kufuata taratibu za nchi.

Hata hivyo, kumekuwa na sintofahamu juu ya usajili wao kutokana na kusajiliwa kama nyota wa kigeni na kuitumikia timu hiyo katika duru la kwanza la Ligi Kuu, na sasa baada ya kudaiwa wamebadili uraia watatambulika vipi wakati dirisha la usajili lilishafungwa tangu Januari 15, mwaka huu.

Uongozi wa klabu hiyo umethibitisha kuwa umeshawasilisha nyaraka za wachezaji hao TFF na kwamba uamuzi wa kuwapitisha kama wazawa au la – upo chini ya kamati hiyo inayotarajiwa kukutana kusikiliza mashauri mbalimbali.

Inaelezwa hatma yao kutambulika katika usajili na namna watakavyotumika duru la pili vipo mikononi mwa kamati hiyo, lakini mabosi wa shirikisho hilo wanaonekana kukwepa kulizungumzia kwa undani.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Said Soud alisema kutakuwa na kikao leo kujadili masuala mbalimbali, ingawa yatakayozungumzwa hakuweza kuyaweka.

“Yapo mambo mbalimbali yatakayojadiliwa, lakini siwezi kusema moja kwa moja tunaenda kujadili nini kwa sababu hadi sasa sijapata mwongozo wa hilo. Uamuzi wote utatolewa baada ya kila kitu kukamilika kwa kusikiliza mashauri yaliyoletwa.”

Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko TFF, Boniface Wambura alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alikiri ni kweli kutakuwa na kikao kupitia masuala mbalimbali hasa yanayohusu wachezaji walioingia dirisha dogo la Januari.

“Siwezi kusema moja kwa moja kama suala la wachezaji hao watatu wa Singida litakuwepo na litajadiliwa kwa sababu uamuzi yote na kujua kitakachojadiliwa yatawekwa wazi baada ya kikao hicho kumalizika hivyo, tusubiri kitakachotokea,” alisema.

Chanzo cha ndani kutoka ndani ya Singida ambacho kiliomba kuhifahidhiwa jina lake gazetini, kililiambia Mwanaspoti ni kweli wachezaji hao waliwasilisha nyaraka zao zote kwa TFF kama wazawa, tofauti na sasa wanavyotambulika kama wageni.

“Klabu yetu iliingiza majina yao kwenye mfumo kama wachezaji wazawa badala ya wageni, taarifa zinaeleza suala hilo liko pia TFF na litatolewa uamuzi kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya timu hiyo.

Januari 23, mwaka huu, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, SSI. Paul J. Mselle, alitoa taarifa kwa Umma kwamba, wachezaji hao watatu waliomba uraia na kupewa kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357.

“Wachezaji tajwa waliomba na kupewa uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357.

“Kwa muktadha huo, Idara ya Uhamiaji inapenda kuutaarifu Umma kuwa watajwa ni raia wa Tanzania kwa Tajnisi,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, SSI. Paul J. Mselle na kuibua maswali juu ya uamuzi huo.

Kanuni ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ibara ya 7 kuhusu kama wachezaji hao wana vigezo vya kuichezea timu ya taifa zinaeleza, awe amezaliwa katika nchi husika, baba au mama yake wa kibaiolojia azaliwe pia kwenye nchi husika.

Kanuni hiyo ya wachezaji hao kama wanaweza kucheza inaeleza pia, Babu au Bibi yake kibaiolojia awe amezaliwa katika nchi husika, awe ameishi katika nchi husika na kama akiwa na umri chini ya miaka 10, angalau awe ameishi kwa miaka mitatu tu.

Pia kama ana umri wa miaka 10 hadi 18 angalau awe ameishi katika nchi husika angalau kwa miaka isiyopungua mitano na pia kama ana umri wa zaidi ya miaka 18, awe ameishi nchi husika kwa muda usiopungua miaka mitano jambo linalozua maswali. Kwa mujibu wa kanuni hizo ni wazi wachezaji hao hawana vigezo vya kuchezea Tanzania kwa sababu hawajafikisha hata mwaka mmoja tangu watue nchini, licha ya kuelezwa wamepewa uraia huo kwa lengo la kupunguza nyota wakigeni waliokuwepo nao.

Hivi karibuni Simba nayo ilieleza kuwaombea uraia baadhi ya nyota wake.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa Idara ya Uhamiaji haijapokea ombi hilo zaidi ya kusambaa mtandaoni tu.

Related Posts