Dar es Salaam. Mapigano yanayondelea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) yameendelea kusababisha mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo ubakaji wa raia na vurugu kwenye balozi sita nchini humo.
Mapigano hayo yanayohusisha majeshi ya Serikali ya DRC dhidi ya kikundi cha waasi cha M23 ambacho kimetengaza kuuteka mji wa Goma ikiwamo kuushika uwanja wa ndege wa kimataifa uliopo kwenye mji huo.
Kuendelea kwa mapigano hayo kumewafanya viongozi katika Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuitisha vikao vya dharura.
Vikao hivyo vilivyoitishwa juzi Januari 28, 2025 ni Baraza la Amani na Usalama (PSC) la Umoja wa Afrika lililokutana kwa ngazi ya mawaziri, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Kamati ya Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Troika), chini ya mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa mashirika ya haki za binadamu yamekishutumu kikundi cha M23 kwa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji na ubakaji wa raia.
Taarifa za Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) zinaeleza zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutokana na mapigano hayo.
Pia, mashirika ya misaada yalisema kuwa hospitali zimefurika mamia ya watu waliojeruhiwa katika mapigano wakiwemo watoto.
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa usambazaji wa misaada ya chakula umesitishwa kwa muda ndani na karibu na mji huo kutokana na mapigano hayo.
Pia, Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu, Jens Laerke amesema kulikuwa na miili mingi ya watu waliouawa mitaani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kati ya waliouawa ni bondia maarufu wa DRC, Balezi Bagunda.
Pia, Shirika la Msalaba Mwekundu limetoa tahadhari kuwa kuendelea kwa mapigano kwenye mji wa Goma kunahatarisha kuenea kwa magonjwa hatari, ikiwemo Ebola, ikiwa maabara zinazohifadhi sampuli za virusi hivyo zitaharibiwa na vurugu.
Katika mji mkuu wa Kinshasa, waandamanaji wamekusanyika na kuchoma moto mbele ya balozi mbalimbali za mataifa ya Magharibi na Afrika, ikiwemo Rwanda.
Ofisi zingine za ubalozi zilizovamiwa na waandamaji hao ni za nchi za Uganda, Kenya, Ufaransa, Marekani na Ubelgiji.
Waandamanaji hao walikuwa wanadai hatua zichukuliwe dhidi ya mashambulizi ya waasi wa M23 katika mashariki mwa DRC.
Pia, mapigano hayo yamesabisha vifo vya watu zaidi ya 25 huku 367 wakijeruhiwa kutokana na majibizano ya risasi mjini Goma.
Mbali na mauaji ya raia pia wanajeshi wa kulinda amani kutoka Afrika Kusini wameripotiwa kuuawa kwenye mapigano hayo na Serikali ya nchi hiyo imethibitisha.
Mji wa Goma ni kitovu cha biashara katika miji iliyopo mashariki mwa DRC.
Kuendelea kwa mapigano yao kumeilazimu Serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC kuandika barua kwenye Baraza la Amani na Usalama (PSC) la Umoja wa Afrika (AU) akiomba kuitishwa kwa mkutano wa dharura.
Mkutano huo uliofanyika Januari 28, 2025 kwa ngazi ya mawaziri ambao walikutana kujadili kuendelea kwa mapigano kwenye eneo la Goma.
Iliezwa PSC itasikiliza maoni kutoka kwa wawakilishi wa Angola ambao ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Tanzania ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Troika) na Kenya ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Pia, PSC ilitarajiwa kupokea taarifa kutoka kwa Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika DRC na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kudumisha Amani DRC (Momusco).
Rais Felix Tshisekedi ndiye Mwenyekiti wa SADC, wakati Rwanda ambayo haiko SADC ni wanachama wa EAC na mwenyekiti wake ni Rais William Ruto wa Kenya.
Tamko la mkutano wa PSC linatarajiwa kulaani ukiukwaji wa mkataba wa kusitisha mapigano, likitaka kusitishwa kwa mapigano na kuondolewa kwa M23 kutoka maeneo iliyoyateka.
PSC pia inaweza kupendekeza kuanzishwa kwa chombo cha usimamizi wa mkataba wa kusitisha mapigano na kuhimiza mazungumzo zaidi chini ya Mchakato wa Luanda.
Baraza hilo linatarajiwa pia kutoa wito wa kuheshimiwa kwa mamlaka na mipaka ya DRC, kuzitaka Rwanda na DRC kujizuia dhidi ya hatua zinazoweza kuchochea mgogoro zaidi na kupendekeza kutumwa kwa ujumbe wa ngazi ya juu kwa Kinshasa na Kigali ili kusaidia upatanishi wa haraka.
Rwanda inadaiwa kuunga mkono kikundi cha waasi cha M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.
Hayo yakiendelea, taarifa zilizopatikana leo Jumatano Januari 29, ni kuwa wakati nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa, zimekemea kitendo cha Rwanda kuliunga mkono kundi la waasi la M23, Serikali ya Marekani imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafakari hatua za kusitisha mapigano hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ameliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutafakari hatua za kusitisha mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wa Rwanda na waasi wa M23 mashariki mwa DRC, huku mgogoro huo ukizidi kupamba moto.
Amesema kuwa Marekani inataka kusitishwa kwa mapigano hayo na kuzitaka pande zote kuheshimu mipaka ya ardhi ya taifa huru.
Pia, ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa, DRC umewataka raia wake kuondoka katika mji wa Goma kwa sababu ya ongezeko la ghasia.
Pia, Serikali ya DRC ilituma barua kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Desemba 17, 2024 ikilaumu Rwanda kwa kuchelewesha mazungumzo kwa kushinikiza mazungumzo ya moja kwa moja na M23.
Rwanda ilikanusha shutuma hizo kupitia majibu yake ya Desemba 19, 2024.
Baraza la Usalama lilipokutana kwa dharura kwa mara ya pili ndani ya siku tatu kujadili hali inayozidi kuzorota DRC, ilielezwa mashambulizi yanayoongezeka ya kundi la M23 yanaendelea kuua raia na askari wa kulinda amani ndani na karibu na jiji la Goma.
Kikao cha dharura cha Troika
Kufuatia kuendelea mapigano, Mwenyekiti wa Troika, Rais Samia Suluhu Hassan naye juzi aliitisha mkutano wa dharura.
Mkutano huo ulifanyika Januari 28, 2025, Ikulu Jijini Dar es Salaam, huku mapigano hayo yakitajwa kuwa sababu ya mkutano huo.
Mkutano huo ulioongozwa na Rais Samia, ulihudhuriwa na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera.
Pia, ulihudhuriwa kwa njia ya mtandao na marais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Felix Tshisekedi wa DRC.
Pia, viongozi wa Afrika Mashariki wanapanga kukutana chini ya mwenyekiti wake Rais wa Kenya, William Ruto.
Tangu 2012, kundi la M23 limekuwa tishio katika maeneo ya Kivu na Ituri, ambapo ilizidi kuimarisha harakati zake za kijeshi tangu Machi 2022.
Katika Mkutano wa Dharura wa AU Mei 2022, Rais wa Angola, João Lourenço, aliteuliwa kuwa msuluhishi wa mgogoro baina ya Rwanda na DRC.
Ingawa alifanikiwa kusaidia kufanikisha mkataba wa kusitisha mapigano Julai 2024, mazungumzo yaliingia kwenye mkwamo Desemba 2024.
Kikao cha ana kwa ana kati ya Rais Tshisekedi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kilipaswa kufanyika Desemba 15, 2024, lakini kiliahirishwa dakika za mwisho kwa ombi la mmoja wa wahusika.
DRC imekuwa ikikumbwa na machafuko ya wanamgambo kwa miongo kadhaa, likiwamo kundi la waasi la M23 linalodai kutetea masilahi ya jamii za wachache wanaozungumza Kinyarwanda, wakiwemo Watutsi.
Tangu mwaka 2022, Kundi la M23 lilianzisha uasi mpya dhidi ya Serikali ya DRC, ikiteka maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini, mkoa unaopakana na Rwanda na Uganda.
Kwa miezi kadhaa, waasi wamekuwa wakidhibiti Rubaya, mji wa madini wenye mojawapo ya akiba kubwa zaidi ya madini ya coltan duniani, madini yanayotumika katika utengenezaji wa simu za mkononi.
Ripoti ya Desemba kutoka kwa Kundi la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilisema kuwa angalau tani 150 za coltan zilisafirishwa kimagendo hadi Rwanda na kuchanganywa na madini ya Rwanda.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa: “Tangu Aprili mwaka 2024, M23 kwa msaada wa RDF (Jeshi la Ulinzi la Rwanda), imepata mafanikio ya kidhibiti maeneo mapya.”
Hata hivyo, Rwanda imekanusha madai hayo, ikisema kuwa mgogoro huo unahusisha masuala ya ndani ya DRC.
Goma ni mji mkubwa zaidi wa Kivu Kaskazini na ni makazi ya takriban watu milioni mbili.
Ni mji wa kimkakati, wenye uwanja wa ndege wa kimataifa na upakana na Ziwa Kivu, unaofungua njia rahisi kuelekea Kivu Kusini na Rwanda.
Pia, Goma ni kitovu cha shughuli za misaada ya kibinadamu kote mashariki mwa DRC.