Mapendekezo, matumaini kwa ARV baada ya katazo la Trump

Dar es Salaam. Licha ya uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha misaada ya maendeleo nje ya nchi hiyo kuwa tishio kwa upatikanaji wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV) bila malipo, wadau wameonesha matumaini ya kuendelea kupatikana kwa dawa hizo.

Matumaini ya wadau hao yanatokana na kile walichoeleza, si Marekani pekee aliyekuwa anatoa msaada wa dawa hizo, Global Fund na washirika wengine ndani ya Shirika la Afrika Duniani (WHO) walikuwa wanatoa.

Kama hatua za kuukabili utegemezi wa misaada nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetaka kuwe na mpango wa dharura wa kisera na kibajeti kugharimia dawa hizo kwa ajili ya waathirika wa Ukimwi.

Kwa upande wa Chama cha ACT Wazalendo, kimeitaka Serikali ipunguze matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha kwenye sekta ya afya, kadhalika ianzishe mfuko wa huduma za afya kitaifa kufadhili mfumo wa afya unaojitegemea.

Maoni ya wadau hao, yanakuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Trump atangaze kusitisha misaada hiyo na kuondoa ufadhili wa Marekani ndani ya WHO, hatua zinazohofiwa kuhatarisha ustawi wa baadhi ya mataifa yaliyokuwa yakitegemea misaada hiyo.

Uamuzi wa kusitishwa kwa misaada hiyo umeenda sambamba na tamko la kukomesha hata miradi iliyokuwa inaendelea kufadhiliwa na nchi hiyo isimame mara moja.

Mshauri wa Masuala ya Afya, Dk Elisha Osati akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Januari 29, 2025 amesema ingawa hatua ya Trump inaibua wasiwasi kwa mataifa yaliyokuwa yanategemea misaada, lakini upande wa ARV Tanzania pengine isiathirike.

Hiyo inatokana na kile alichofafanua, sio Marekani pekee iliyokuwa inaisaidia Tanzania dawa za ARV, bali Global Fund na washirika wengine kutoka WHO walikuwa wanatoa.

“Kikubwa ARV hazitoki Marekani tu, zinatolewa pia na Global Fund hiyo ndio inayotupa matumaini. Global Fund pia inatoa fedha za kifua kikuu na malaria hiyo inatupa matumaini,” amesema.

Hata hivyo, amesema athari za uamuzi huo, hazitaiangukia Afrika pekee kuna mashirika yasiyo ya kiserikali Marekani yanayojiendesha kwa kusaidia programu za afya za mataifa ya Afrika nayo yataathirika.

“Iwapo katazo hilo litatekelezwa litaleta matatizo makubwa katika programu nyingi tunazofanya. Lakini naona kwa sasa majaji wa Marekani wameonyesha nia ya kusitisha kwa muda katazo hilo ili kutoa nafasi ya majadiliano,” amesema.

Kupitia taarifa ya ACT-Wazalendo iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Wananchi Chadema, Ashura Masoud amesema Serikali inapaswa kuandaa mkakati wa dharura wa kisera na kibajeti kuhakikisha inakuwa na fedha ya kutosha kwenye mfuko wa kudhibiti Ukimwi.

Pia, ametaka Bunge linapaswa kulijadili jambo hilo kwa dharura na Serikali iwasilishe bungeni taarifa ya tathimini na mkakati wa kina wa namna ya kukabiliana na upungufu wa fedha katika sekta zote.

“Rais ashauriane na wakuu wenzake wa nchi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Afrika (AU) ili ufanyike mkutano wa wakuu wa nchi kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi,” imeeleza taarifa hiyo.

Amesema idadi ya waathirika wa VVU hadi sasa wanaofaidika na misaada ya dawa za kufubaza VVU ni takriban milioni 1.5 na wastani wa Sh204 bilioni kwa mwezi mmoja hutumika.

Ameeleza kwa tathimini waliyoifanya, wameona uamuzi wa Marekani utaathiri huduma ya ARV na mapambano ya VVU kwa zaidi ya asilimia 50.

Ashura kupitia taarifa hiyo, imemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Dare, Dk Lilian anayeitaka Tanzania kujiandaa vilivyo kwani uwezo wake wa kuchangia ARV, VVU na Ukimwi ni asilimia sita pekee kupitia bajeti ya Wizara ya Afya na mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF).

Kwa upande wa Waziri Kivuli wa Afya wa ACT- Wazalendo, Dk Elizabeth Sanga ameitaka Serikali ipunguze matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha kwenye huduma za afya.

Amependekeza kuanzishwe mfuko wa huduma za afya ya kitaifa kwa kutumia rasilimali za ndani kama madini na utalii kufadhili mfumo wa afya unaojitegemea.

“Serikali iongeze bajeti ya afya kutoka wastani wa asilimia 5.7 hadi kufikia asilimia 10 ya bajeti kuu 2025/2026, ili kupunguza utegemezi na kuboresha huduma za afya,” amesema.

Ameitaka Serikali iharakishe utekelezaji wa mfumo wa kuwaunganisha Watanzania na Hifadhi ya Jamii na kutoa bima ya afya kwa wote ili kuongeza uwezo wake kugharamia,  na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi wa kifedha.

Related Posts