Migogoro ya ardhi, ndoa, ukatili mfupa mgumu

Mikoani. Migogoro ya ardhi, ndoa, na unyanyasaji wa kingono vimetajwa kuwa miongoni mwa malalamiko makubwa ya wananchi katika kipindi hiki cha Wiki ya Sheria, huku wananchi wakiomba Serikali na vyombo vya kisheria kuweka mfumo rasmi wa kutatua changamoto hizo.

Wiki ya Sheria inaendelea katika maeneo yote nchini kwa kusikiliza malalamiko na kutatua kero za wananchi, ambapo maadhimisho hayo yanatarajiwa kufikia tamati Februari 3, mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo, Januari 29, 2025 baadhi ya wananchi mkoani Mbeya wamesema migogoro ya ardhi, ukatili, na ndoa imekuwa mingi, hivyo wanaiomba Serikali kutafuta njia muafaka ya kuikomesha.

Baadhi yao wamesema hata vitendo vya mauaji vinaendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali nchini.

Victoria Mwasekaga, amesema kuwa migogoro ya ardhi, hasa katika mashamba yaliyopo karibu na ofisi za mamlaka za Serikali na hifadhi, imekuwa sugu, akiomba sheria zichukue mkondo wake.

“Unakuta mtu amezaliwa na kukulia eneo fulani, baadaye serikali inaona eneo hilo linafaa kwa ofisi yake. Badala ya kukaa meza moja ya mazungumzo, inatumika nguvu,” amesema Victoria.

Josiah Abel, amesema kuwa sheria za ardhi bado hazifuatwi ipasavyo, kwani wenye kipato cha juu wanapewa kipaumbele huku wasio na uwezo wakidhulumiwa haki zao.

“Kama kweli mahakama ipo kwa ajili ya kutoa haki, basi isaidie wanyonge. Tunadhulumiwa ardhi kwa sababu hatuna uwezo wa kifedha. Mtu mwenye fedha anapotaka eneo kwa shughuli zake, anatuondoa,” amesema Abel.

Neema Mwasika, amesema kuwa Serikali inapaswa kupitia upya utaratibu wa wanandoa kutoa talaka.

“Sasa hivi wanawake wanaachika kiholela. Ukianza mchakato wa talaka, unachukua muda mrefu. Naomba serikali ipitie upya sheria ili haki itendeke,” amesema Neema.

Hamis Mang’andu (85), mkazi wa jijini Tanga, amesema kuwa ucheleweshaji wa kesi, kuhamisha mashauri, na uzembe wa mawakili katika kufuatilia kesi, kunasababisha wananchi kukosa haki zao.

“Kutokuwa na elimu ya sheria kumesababisha tusilipwe mafao yetu ya zaidi ya Sh4.3 bilioni za kiinua mgongo kwa kipindi cha miaka 26. Wenzetu wengi wamefariki dunia bila kupata haki zao. Tunaomba msaada,” amesema kikongwe huyo.

Mahakama yakiri malalamiko

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Joachim Tiganga, amekiri kuwa malalamiko mengi yanayopokelewa ni kuhusu migogoro ya ardhi, mirathi, na ukatili wa kijinsia, hasa katika shule na vyuo.

Amesema kuwa kero nyingine zinazowakabili wananchi ni utoaji wa vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa, vyeti vya kifo, pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).

“Kutokana na malalamiko haya, lengo letu ni kutoa elimu, kusikiliza na kutatua changamoto hizi kwa kushirikiana na mamlaka nyingine kama RITA,” amesema Jaji Tiganga.

Ameongeza kuwa kuna mifumo mipya ya kielektroniki ya usikilizaji wa mashauri ambayo inamwezesha mwananchi kufungua na kufuatilia kesi akiwa nyumbani na kupata taarifa ya mwenendo wa shauri lake.

“Tunataka kuona mabadiliko chanya. Tunasikiliza kero za wananchi wote bila kujali hali yao ya kiuchumi au elimu. Hakuna sababu ya mtu kujichukulia sheria mkononi, bali afuate taratibu zilizowekwa,” amesema.

Amefafanua kuwa katika kutekeleza hilo, maofisa wa mahakama wamesambazwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Mbeya na Songwe ili kuwafikia wananchi, huku akisisitiza kuwa huduma hizo zinatolewa bure.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Hudi Majid Hudi, amesema kuwa migogoro ya kazi katika sehemu za kazi pia ni mojawapo ya malalamiko yanayojadiliwa kwa kina.

“Malalamiko mengine tunayopokea ni ya migogoro ya ardhi, unyanyasaji wa kijinsia, na ndoa. Tunajitahidi kutoa elimu na kutafuta suluhisho,” amesema Hudi.

Wakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Marco Minja, amesema kuwa wastaafu wengi wamekuwa wakikosa haki zao kutokana na kukosa msaada wa kisheria.

“Ndiyo maana tupo hapa kutoa elimu kuhusu masuala ya sheria ili wananchi wajue wapi pa kuanzia wanapofuatilia haki zao mahakamani,” amesema Minja.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Adelina Ngwaya, amewaomba wananchi kutumia Wiki ya Sheria kujifunza masuala mbalimbali ya sheria.

Amesema wanatumia muda huo kuwafikia wananchi katika mikusanyiko mbalimbali ili kutoa elimu na kuwawezesha kufahamu haki na majukumu yao kisheria.

“Wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya sheria. Unakuta mtu anapeleka kesi mahakamani, kisha anashangaa kwa nini shauri lake limesomwa katika kesi ya madai badala ya jinai,” amesema Ngwaya.

DCEA yakanusha upotevu wa ushahidi

Ofisa Sheria Mwandamizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Batilda Mushi, amesema hakuna vielelezo vya watuhumiwa waliokamatwa na mamlaka hiyo vilivyopotea mikononi mwao.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya Wiki ya Sheria katika Viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma, Batilda amesema kuwa mfumo mzuri wa utunzaji wa vielelezo umewekwa ili kuhakikisha ushahidi unatumika ipasavyo mahakamani.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ipyana Mlilo, amehoji upotevu wa ushahidi wa watuhumiwa wa dawa za kulevya unaoripotiwa mara kwa mara.

“Kwa sababu tunasikia kuna baadhi ya watuhumiwa wanaokamatwa na madawa ya kulevya wanaachiwa huru kwa sababu ushahidi unakuwa umepotea mikononi mwenu,” amehoji Mlilo.

Akijibu swali hilo, Batilda amesema kuwa DCEA ina mfumo madhubuti wa kutunza ushahidi tangu mtuhumiwa anapokamatwa hadi anapofikishwa mahakamani, hivyo si rahisi ushahidi huo kupotea.

“Tunajua kuwa ushahidi ni muhimu katika utoaji wa hukumu stahiki, hivyo tunahakikisha kuwa tunautunza kwa umakini mkubwa,” amesema.

Imeandikwa na Saddam Sadick (Mbeya), Burhan Yakubu (Tanga), Christina Thobias (Iringa) na Rachel Chibwete (Dodoma).

Related Posts