Rais Samia kuzindua sera ya elimu na mafunzo

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan atazindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, inayolenga kuleta mageuzi makubwa katika elimu nchini.

Miongoni mwa mageuzi yaliyopo kwenye sera hiyo ni kufundishwa kwa somo la Tehama, mafunzo ya ufundi stadi kuanzia elimu ya msingi, na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence – AI).

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ameyasema hayo leo Jumatano, Januari 29, 2025, alipozungumzia uzinduzi wa sera hiyo utakaofanyika Ijumaa, Januari 31, 2025, jijini Dodoma.

Msigwa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema lengo la mapitio ya sera hiyo ni kuwafanya wanafunzi kuwa na umahiri na ujuzi unaoakisi mahitaji kitaifa na kimataifa ili kushindana na kushiriki kikamilifu kwenye soko la ajira duniani.

Amesema sera hiyo itazalisha wanafunzi wenye maarifa, maadili, na ujuzi utakaowawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali kujiajiri, kuajiri wengine, na kuongeza uwezo wa ushindani kwenye soko hilo.

“Mapitio hayo yanaendana na utekelezaji wa Ilani ya CCM kuhusu kuimarisha huduma za kijamii, ambapo imejielekeza kuhakikisha kila rasilimali watu inakuwa na ujuzi,” amesema.

Amebainisha kuwa mapitio hayo yameshirikisha wadau mbalimbali na matokeo makubwa yanatarajiwa, kwa kuwa huduma ya elimu inagusa moja kwa moja jamii.

Amesema Rais Samia alitoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya kazi kubwa ya kupitia Sera ya Elimu, kwa lengo la kuwa na sera inayowaandaa wanafunzi kuwa mahiri katika kukabiliana na changamoto za sasa na kujibu mahitaji ya dunia ya sasa.

Amesisitiza kuwa Rais hakupendezwa na hali ya wanafunzi kuhitimu shahada huku wakiwa hawana ujuzi wa uzalishaji.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema sera hiyo itazinduliwa sambamba na vitendea kazi, ikiwamo mkakati wa utekelezaji wa sera ambao tayari umeandaliwa.

Aidha, amesema sera hiyo imeelekeza kuboresha mitaala ya elimu, ambayo tayari imeboreshwa kwa ngazi zote, kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vikuu, ambapo kwa sasa vyuo hivyo vinaendelea na maboresho zaidi.

Amesema mitalaa hiyo inahusisha elimu ya awali, elimu ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, elimu ya sekondari ngazi ya chini na juu, pamoja na mafunzo ya ualimu, ambayo imeanza kutumika mwaka jana na matunda yake yameanza kuonekana.

Mbali na hilo, amesema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, sekta ya elimu kupitia sera hiyo imeandaa mkakati wa matumizi ya Tehama katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Related Posts