Imefichuka! Ujanja wa Fadlu uko hapa tu

KIKOSI cha Simba kinajiandaa kuondoka Dar es Salaam kwenda Tabora kwa ajili ya pambano la kiporo cha Ligi Kuu Bara, huku kikiwa kinaongoza msimamo wa ligi hiyo, lakini ikianikwa siri zinazombeba kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids.

Simba itavaana na Tabora United inayoelezwa baadhi ya nyota wake wapya waliosajiliwa dirisha dogo wakiwa hawajapata vibali kama ilivyokuwa timu hiyo katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa msimu wa msimu huu dhidi ya Wekundu hao na kujikuta wakilala mabao 3-0 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakati Wekundu wakijiandaa kupaa kwenda Tabora, imebainika jukumu la ufundi na upangaji wa kikosi hicho lililopo chini ya Fadlu, lakini maujanja yote yanayoifanya timu hiyo itishe yapo kwa watu anaofanya nao kazi Msimbazi.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Inaelezwa kuna watu wanne ambao kutokana na unyeti wa majukumu yao wamekuwa na nafasi kubwa ya kuamua nani acheze na nani asicheze, hivyo kumfanya Fadlu kuwa mfanya uamuzi wa mwisho tu katika mechi yoyote iwe kwa ligi ya ndani au ile ya kimataifa.

Mwanaspoti limebaini kuwa upangaji wa kikosi wa Fadlu umekuwa ukitegemea watu hao wanne muhimu na bila hao kupitisha jina la mchezaji, ni vigumu kwa kocha huyo Msauzi kumpa nafasi kikosini.

Mtu wa kwanza ni daktari wa timu Edwin Kagabo aliye mkuu wa Idara ya Afya na Tiba ambaye ripoti yake humpa mwongozo Fadlu wa hali za kiafya za wachezaji kabla hawajatumika katika progamu za mechi au mazoezi. Ukimuweka kando Kagabo, mtu mwingine ambaye ana nguvu kubwa ya ushawishi katika upangaji wa kikosi ni kocha wa mazoezi ya viungo ya timu hiyo, Riedoh Berdien ambaye humpa Fadlu ripoti za utayari wa kimwili wa kila mchezaji aliyeshiriki programu za mazoezi wakati wa kujiandaa na mechi husika, ambapo wachezaji ambao huonyesha ufanisi huwa na uwezekano mkubwa wa kuanza kikosini.

Mtu wa tatu ni mtathmini wa video na viwango wa timu, Mueez Kajee ambaye humpa muongozo wa mchezaji gani anastahili kuanza kulingana na mbinu ambazo amepanga kuzitumia katika mchezo na ubora na aina ya wachezaji wa timu pinzani wanayocheza nayo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Fadlu pia amekuwa akimtegemea meneja Patrick Rweyemamu anayetunza rekodi na takwimu za kinidhamu za wachezaji na ndiye wa kwanza kufahamu idadi ya kadi kwa kila mchezaji na nani anaweza kutumika au kutotumika iwapo kuna adhabu ya kutotumika au la.

Akizungumzia hilo, winga wa zamani wa Simba, Yusuph Mgwao alisema soka la kisasa linalazimisha muundo unaotumiwa na Simba.

“Kwa sasa kocha anakuwa ni kama meneja na nyuma yake kunakuwa na kundi kubwa la maofisa ambao wanatekeleza majukumu tofauti ambayo anakuwa anawapa, maana yeye hawezi kufanya kazi zote peke yake.

“Hili ni jambo zuri kuona timu zetu sasa zinakuwa na benchi pana la ufundi na ndio maana zimekuwa zikifanya vizuri kimataifa kulinganisha na zamani,” alisema Mgwao.

Katika hatua nyingine, Simba inatarajia kuanza wiki tatu ngumu mwezi ujao ikikabiliwa na michezo sita ya Ligi Kuu Bara, huku hesabu za Fadlu zikielekezwa mechi dhidi ya Tabora United itakayopigwa Jumapili hii.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Simba inaingia katika mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, ikiwa na nguvu baada ya kutoka kuifunga Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro mabao 6-0 katika mzunguko wa 64, wa Kombe la Shirikisho la FA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dar es Salaam, Fadlu alisema wanaenda kwa tahadhari akiweka wazi malengo ni kuondoka na pointi tatu ugenini, huku akidai mzunguko wa pili utakuwa mgumu kwa kila timu. “Tunahitaji kuendelea kuonyesha ubora katika raundi ya pili, kipindi hiki kitakuwa kigumu kwa sababu ya namna michezo ilivyokuwa karibu. Hata ukiangalia pia gepu la pointi na wapinzani wetu sio kubwa hivyo ni lazima tujipange,” alisema.

Kocha huyo ambaye ameipeleka Simba robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu ikiwa ni misimu sita kati ya saba ya klabu Afrika tangu 2018, alisema kasi ya ushindani ni chachu nzuri kwao ya kuendeleza ubora walionao.

Wakati Fadlu akizungumza hayo, kwa upande wa Tabora United huenda isiwatumie nyota wapya wa kigeni ambao imewasajili dirisha dogo kwa kile kinachoelezwa miongoni mwao kukosa leseni kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.

Nyota wanaotajwa ni kipa Jean-Noel Amonome aliyetoka AS Arta/Solar7 ya Djibouti, winga, Joseph Akandwanaho aliyetoka Mbarara City ya kwao Uganda na kiungo mkabaji raia wa Cameroon, Martial Zemba Ikoung kutokea Union Touarga Sportif.

Hata hivyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Tabora United, Christina Mwangala alipotafutwa kuhusiana na suala hilo alisema hawezi kuzungumzia kitu cha kusikia ambacho hakina uhalisia.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kocha wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi alisema hana presha kuhusiana na mchezo huo akisisitiza kuwa wamejipanga licha ya kusifu kiwango cha wapinzani wao.

Mchezo huo ni wa kisasi kwa wenyeji ambao mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam, Agosti 18, mwaka jana, Simba ilishinda mabao 3-0, yaliyofungwa na Che Malone Fondoh, Valentino Mashaka na Awesu Awesu.

Related Posts