Walibya watenga Sh 3B kwa Mzize, mchongo mzima upo hivi

SIKU chache baada ya kuripotiwa kwamba mabosi wa Yanga wamelegeza kamba kwa kuwa tayari kumuuza mshambuliaji nyota Clement Mzize, matajiri wa Klabu ya Al Ittihad ya Libya wameamua kufanya kweli kwa kumuwekea mezani ofa ya mabilioni ya shilingi.

Awali mabosi wa Yanga, walizikaushia ofa kadhaa zilizotua kutaka kumnunua Mzize, lakini hivi karibuni mmoja wa vigogo alilithibitishia Mwanaspoti kwamba, kwa sasa wapo tayari kumuuza na hii ni baada ya klabu moja ya Ubelgiji kuweka mezani zaidi ya Sh2.5 bilioni ili kumnyakua.

Lakini kabla mambo hayajakaa vizuri, taarifa mpya kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba Al Ittihad imetoa ofa ya maana kupitia kwa wakala iliyemtafuta ili kuiunganisha na menejimenti ya mchezaji huyo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Katika mazungumzo inaelezwa kwamba Al Ittihad imepanga kumpa Mzize mkataba wa miaka miwili wenye ada ya usajili ya Sh650 milioni kwa mwaka, ikiwa na maana ya miaka miwili nyota huyo atavuna zaidi ya Sh1 bilioni.

Pia inaelezwa klabu hiyo imepanga kumlipa mchezaji mshahara wa Sh50 milioni kwa mwezi kama dili hilo litatiki, huku ikidaiwa Yanga imetengewa Sh3 bilioni ili kumuuza na inasemekana Yanga wako tayari kupokea kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, Mwanaspoti iliwasiliana na Makamu wa Rais wa Yanga, Haji Arafat aliyesema hana taarifa ya ofa hiyo na kama itakuwepo watatoa taarifa kwa umma.

“Kwa kweli kama ofa hiyo imekuja bado sijaisikia labda kama ilikuja usiku wa jana (juzi) au asubuhi hii (jana). Ila ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho kwa sasa, lakini ngoja nifuatilie,” alisema Arafat aliyekiri kuwepo kwa ofa za awali.

Awali mmoja wa vigogo wa Yanga alikiri kwamba wako tayari kumuuza Mzize kutokana na kupokea ofa nyingine na baadhi zikiwa zimevuka kiwango walichokiweka cha Sh2 bilioni walizokuwa wakitaka wapewe ili wamuachie.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Ofa za awali zinadaiwa zilikuwa zimetoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Wydad Casablanca ya Morocco waliorejea mara mbili wakiongeza dau walilolitanguliza mapema la Sh1.5 bilioni hadi bilioni mbili, huku lile la klabu kutoka Ubelgiji ambayo hata hivyo haitajwi likiwavutia zaidi kwani dau ni Sh2.5 bilioni.

Nyota huyo mwenye miaka 21 amekuwa gumzo Afrika kutokana na kiwango alichoonyesha katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika tangu msimu uliopita. Msimu uliopita Yanga ilifika robo fainali na kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na msimu huu imeishia makundi.

Bao lake dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo zilipokutana Dar es Salaam lilichaguliwa kuwa bora la wiki na kumfanya apae zaidi na kuwa gumzo.

Hata hivyo, licha ya ofa hiyo inadaiwa wasimamizi wake hawapo tayari kumruhusu kwenda huko kwani wanaamini anaweza kufanikiwa zaidi akienda Ulaya hususan Ubelgiji.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

“Tatizo ni menejimenti yake kwani inaamini Mzize anaweza kupata ofa zaidi kuliko hiyo, hivyo ni kama wanataka kuipotezea ofa hii ya Al Ittihad,” kilisema chanzo hicho. Meneja wa Mzize, Yasmine Razack anayetajwa kuwa mtu mwenye mawasiliano makubwa na familia ya mpira Ulaya, jana hakupatikana kufafanua juu ya ofa hiyo na iwapo wameamua kuikaushia ili kusubiri ofa zaidi kutoka Ulaya.

Related Posts