MAAFANDE wa KVZ na KMKM zimeaga michuano ya Kombe la Shirikisho Zanzibar (FA) baada kushindwa kufurukuta katika mechi za robo fainali ya michuano hiyo.
KVZ iling’olewa jana Jumatatu kwa kufungwa na Mlandege kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 la pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Mao, mjini Unguja kumalizika kaa suluhu.
Katika mechi nyingine ilipigwa Mao B, watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) KMKM walifumuliwa kwa mabao 4-0 na Uhamiaji na kuaga michuano hiyo.
Leo jioni katika mechi nyingine za robo fainali, Zimamoto iliwazima Mafunzo kwa bao 1-0, huku vinara wa Ligi Kuu na watetezi wa michuano hiyo ya FA, JKU ikiitambia Taifa Jang’ombe kuifunga penalti 4-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.
Timu hizo nne zilizofuzu nusu fainali ya michuano hiyo kwa sasa zinasikilizia ratiba ya hatua hiyo, ili kujua zitakutana vipi kusaka tiketi ya fainali.
Bingwa wa michuano hiyo ndio anayeiwakilisha Zanzibar katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Msimu uliopita JKU ilitwaa taji hilo kwa kuifunga Chipukizi kwa mabao 2-0 katika mechi kali ya fainali na kushiriki michuano ya CAF ikitolewa raundi ya kwanza na Singida Big Stars kwa jumla ya mabao 4-3.
Singida ilishinda mechi ya kwanza kwa mabao 4-1 kabla ya JKU kujitutumua ziliporudiana kwa kushinda 2-0, lakini ikakwama kusonga mbele.
Hata hivyo, Singida ilitolewa raundi ya pili na Future ya Misri kwa jumla ya mabao 4-2 kwani ilishinda nyumbani kwa bao 1-0 na kwenda kulala ugenini 4-1.