Bunda. Asilimia 32 ya wanafunzi waliopangiwa kujiunga na kidtao cha kwanza katika shule mbalimbali za Sekondari wilayani Bunda katika Mkoa wa Mara bado hawajaripoti shuleni licha ya shule hizo kufunguliwa takriban wiki mbili sasa.
Aidha asilimia 36 ya wanafunzi waliotarajiwa kuanza darasa la kwanza wilayani humo pia bado hawajaripoti huku asilimia 42 ya wanafunzi wa madarasa ya awali pia wakiwa bado hawajaripoti shuleni.
Takwimu hizo zimetolewa leo Januari 30, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dk Vicent Naano alipokuwa akipokea vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh8 milioni kutoka kwa kampuni ya Grumeti Reserves kwaajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa na ofisi ya mtendaji kwa vijiji vya Mihale na Nyamatoke wilayani humo.
Dk Naano amefafanua kuwa jumla ya wanafunzi 4,025 walichaguliwa kujiunga na shule za sekondari wilayani humo lakini hadi sasa ni wanafunzi 2,656 ndio wameripoti.
“Kwa darasa la kwanza tulitarajia wanafunzi 5,559 lakini hasa sasa ni wanafunzi 3,587 ndio wapo shuleni na kwa awali tulitarajia wanafunzi 6,059 ila hadi sasa waliopo shuleni ni wanafunzi 3,525,” amesema.
Kufuatia hali hiyo mkuu huyo wa wilaya ametoa maagizo kwa watendaji wa kata na vijiji kuanza msako wa wazazi ambao bado watoto wao hawajaripoti shuleni ili kuwachukulia hatua.
Amesema mzazi atakayekamatwa kwa kushindwa kumpeleka shule mwanawe atatozwa faini ya Sh50,000 na kwamba msako huo unatarajiwa kuanza siku ya Ijumaa.
“Hutataki uzembe kwenye mambo ya muhimu kama elimu, hakuna kikwazo cha mwanafunzi kupelekwa shule kwani tayari nilishaagiza wanafunzi wote wapokelewe hata kama hawana sare za shule, sasa hiki kinachofanyika ni uzembe ambao serikali haiwezi kuvumilia, lazima watoto wote waende shule na hii ni kwa faida ya jamii nzima,” amesema.
Dk Naano Kuhusu msaada uliotolewa na Grumeti mkuu huyo wa wilaya amewataka wasimamizi wa miradi inayotarajiwa kutekelezwa kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo ili iweze kutekelezwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha na kuepuka wizi wa vifaa vya ujenzi katika miradi hiyo.
Amesema wilaya ya Bunda imekithiri kwa wizi wa vifaa vya kwenye miradi na kwamba hatua kali zinaendelea kuchukuliwa dhidi ya wasimamizi wasiokuwa waaminifu.
“Bunda kuna vitendo vya wizi wa vifaa kwenye miradi, tayari kuna watu kadhaa wakiwepo watumishi wa umma ambao wanashikiliwa au wamefikishwa mahakamani kwa kujihusisha na vitendo hivyo,niwaombe wasimamizi wa miradi kuzingatia utaratibu na kuwa waadilifu kwani hatutasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokwenda kinyume,” amesisitiza.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Taasisi ya Grumeti Fund, David Mwakipesile amesema msaada wa vifaa uliotolewa kwa vijiji vya Mihale na Nyamatoke ni utekelezaji wa makubaliano kati ya vijiji hivyo na kampuni hiyo ambapo kampuni hiyo inatakiwa kutoa msaada wa vifaa vyenye thamani ya Sh4 milioni kwa kila kijiji kila mwaka kwaajili ya kutekeleza miradi kwenye vijiji husika.
“Kwa Mihale msaada huu unalenga kusaida katika ujenzi wa madarasa mawili ya shule shikizi ili kuwasaidia wanafunzi wa madarasa ya awali kutokutembea umbali wa zaidi ya kilomita 4 kila siku kwenda na kurudi shuleni wakati kwa Nyamatoke msaada unalenga kusaidia uezekaji wa ofisi ya mtendaji,” amesema.
Mwakipesile amesema msaada huo unahusisha vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na mbao,misumari,mabati na mifuko ya saruji huku akitoa wito kwa wakazi wa vijiji hivyo kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamja na kuepukana na vitendo vilivyokithiri vya uharibifu wa mazingira katika mto Robana Amefafanua kuwa mto huo ambao ni chanzo cha maji katika ikolojia ya hifadhi ya Serengeti sambamba na vijiji 12 vilivyopo katika wilaya za Serengeti na Bunda upo hatarini kutokweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaendelea ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti hovyo.
“Hali ikiendelea hivi huu mto utakauka ndani ya miaka mitano hadi kumi ijayo na mkumbuke kuwa misaada kama hii ni matokeo ya uhifadhi hivyo ni vema sote kwa pamoja tukawa walinzi na mabalozi wema wa uhifadhi ili tuweze kufaidia matunda ya uhifadhi kwa pamoja,” amesema
Wakizungumza kuhusu wanafunzi kutokuripoti kwa wakati shuleni, baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Bunda wamesema hali hiyo inatokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi ya wazazi kuamua kuwapeleka watoto wao katika shule binafsi.
“Wapo wazazi ambao wamewapeleka watoto wao shule za binafsi hivyo wasipoonekana kwenye shule walizopangiwa inaweza kuchukuliwa kuwa wapo nyumbani tu kumbe tayari wapo kwenye shule binafsi ndani ya wilaya au nje ya wilaya,” amesema Modesta Balili.
Morobani Matengu amesema uelewa mdogo juu ya umuhimu wa elimu katika jamii pia unachangia baadhi ya wazazi kuamua kuwazuia watoto wao kutokwenda shule badaa yake kuwashirikisha katika shughuli za utafutaji mali kwaajili ya familia.
“Wapo watoto ambao badala ya kwenda shule wazazi wanawatumia kwenye shughuli za kiuchumi mfano kwenda shambani kulima, kuchunga mifugo au hata kufanya biashara ndogo ndogo ,mimi naunga mkono msako ufanyike wazazi wa aina hii wakamatwe kwani wanawakosesha watoto wao haki ya kupata elimu,” amesema Matengu.