Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma, amesema kifo cha Sheikh Muhammad Iddi kimesababishwa na presha kupanda leo asubuhi Alhamisi Januari 30, 2025, kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Mloganzila na baadaye kufariki dunia akiwa njiani.
“Hali hiyo ilisababisha mishipa ya damu kupasuka na kusababisha damu kutoka na kufariki dunia kabla ya kufikishwa Hospitali ya Mloganzila, ” amesema Jabiri alipozungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu.
Katika maelezo yake, Jabiri amesema kwa sasa visomo na dua mbalimbali vinaendelea kufanyika nyumbani kwake eneo la Buguruni Mnyamani Dar es Salaam.
“Baada ya visomo hivyo mwili utafikishwa katika msikiti wa makao makuu ya Bakwata hapa Kinondoni majira ya saa 10 jioni kwa ajili ya kuuswalia kisha kuandaa safari ya kuusafirisha kwenda Mkata Handeni Tanga kwa maziko kesho,” amesema.
Alhaj Mruma amesema enzi za uhai wake mbali ya kuwa sheikh maarufu jijini Dar es Salaam, alikuwa miongoni mwa wasomi wa Kiislam wanaounda jopo la wanazuoni wa dini hiyo wanaotegemewa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya masuala ya kidini.
“Enzi za uhai wake alikuwa anaendesha vipindi mbalimbali vya somo la dini hiyo katika runinga ya Chaneli ten, lakini pia alikuwa na runinga yake ya mtandaoni,” amesema Jabiri.
Taarifa ya mazishi inaonyesha kuwa mwili wake utaoshwa na kuswaliwa katika Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni leo wakati wa swala ya Adhuhuri, sambamba na visomo vitakavyofanyika msikitini hapo.
Taarifa imeongeza baadaye alasiri, mwili wake utapelekwa makao makuu ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) na kuswaliwa tena kabla ya kusafirishwa kuelekea Mkata kwa maziko yatakayofanyika baada ya Swala ya Ijumaa.
Kitabu chake na mchango kwa jamii
Akiwa maarufu kwa jina la Abu Idd, marehemu atakumbukwa kwa michango yake mbalimbali kwa jamii, kikiwamo kitabu alichokiita kwa jina la Misingi 15 ya Amani.
Katika kitabu hicho, utangulizi wake umeandikwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuberi.
Mwanahistoria na mmoja wa watu wa karibu wa marehemu, Sheikh Mohamed Said alikielezea kitabu hicho kuwa kimetokana na fikra ya mwandishi akikusudia kuwatakia kheri Watanzania ambao dini zao kubwa mbili ni Uislam na Ukristo, imani ambazo ikiwa waumini wake hawatendeana haki na uadilifu katika nafasi zao za maamuzi ndani ya vyombo vya umma na Serikali, amani ya nchi itakuwa hatarini.