Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema kwa sasa haiwezi kuruhusu kituo cha Murusagamba kufanya kazi kwa saa 24 sababu mbili zikitajwa ni udogo wa mwenendo wa bidhaa na watu katika kituo hicho.
Kauli hiyo imetolea bungeni leo Alhamisi Januari 30, 2025 na Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro.
Katika swali la msingi mbunge huyo ametaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuwezesha Vituo vya Forodha vya Murusagamba na Kabanga kufanya kazi masaa 24.
“Kituo cha Murusagamba ni kidogo cha uzuiaji cha forodha (Preventive office), vituo hivi hufanya kazi ya kuzuia magendo kwenye maeneo ambayo mwenendo wa bidhaa na watu ni mdogo. Kutokana na udogo wa mwenendo wa bidhaa na watu katika kituo cha Murusagamba uwezekano wa kituo hiki kufanya kazi masaa 24 kwa sasa haupo,” amesema Chande.
Kuhusu Kituo cha Forodha cha Kabanga amesema ni kituo cha pamoja (OSBP) cha kutoa huduma za forodha baina ya Tanzania na Burundi ambacho kina miundombinu wezeshi kama ikiwemo taa za ulinzi, vyombo vya ulinzi na usalama, na maeneo ya kukagulia bidhaa.
Mingine ni wasafiri na wafanyakazi, hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi saa 24 kwa upande wa Tanzania lakini akasema ili kituo hicho kiweze kutoa huduma saa 24, upande wa Kobero nchini Burundi unapaswa pia kuwa tayari kutoa huduma hizo masaa 24.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, hivi sasa kituo cha OSBP Kobero kwa upande wa Burundi kinatoa huduma kwa saa 12 tu lakini jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika ili kuwezesha mazingira ya kituo cha OSBP Kobero kufanya kazi saa 24, hususan ulinzi na usalama.