Gusa achia yambeba Ramovic Yanga

KOCHA wa Yanga, Sead Ramovic wikiendi hii anaingia tena kibaruani kuiongoza katika mechi ya kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar huku akiwa na silaha inayombeba zaidi katika falsafa yake ya ‘Gusa Achia Twende Kwao’ iliyoonyesha matunda katika mechi tano zilizopita.

Yanga iliyoachwa pointi moja na Simba katika msimamo wa ligi ina nafasi ya kukaa kileleni ikishinda kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Ramovic aliyetambulishwa na Yanga Novemba 15, 2024 akichukua mikoba ya Miguel Gamondi ameiongoza Yanga kucheza mechi tano za ligi na kushinda zote, huku akivuna mabao 18 na kufungwa mawili, akiwa na clean sheet michezo minne.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Hadi sasa, Ramovic ameonekana katika mechi hizo tano za ligi amekifanya kikosi kuwa kigumu kuruhusu bao, lakini safu ya ushambuliaji ikifunga mabao mengi zaidi na katika hilo, kuna mambo matatu yapo nyuma yake.

Wakati mashabiki wa Yanga wakifurahia matokeo hayo na pengine kuona kuna mwanga wa kurudi kilele cha mafanikio na kutetea taji, Ramovic anabebwa zaidi na soka la kushambulia kwa kasi muda mwingi yaani ‘Gusa Achia Twende Kwao’.

Katika kucheza soka hiloi, Ramovic, ameimarisha ubora wa wachezaji kujilinda na kushambulia hali iliyotoa matokeo chanya ya kufunga mabao 11 pekee kipindi cha kwanza na saba kile cha pili kati ya 18 yaliyofungwa kwenye mechi tano.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mbali na hilo, katika mchakato wa kupatikana mabao hayo 18, Prince Dube, Clement Mzize na Pacome Zouzoua wameonekana kuwa ndio waliohusika zaidi kufunga na kutengeneza, unaweza kusema ndiyo injini ya Yanga kufanya pointi tatu zinabaki mikononi mwao.

Takwimu zinaonyesha katika mechi tano za Ramovic kwenye ligi wachezaji hao kila mmoja amehusika kwenye mabao saba – iwe kufunga au kutoa asisti. Dube amefunga mabao matano na asisti mbili, Mzize manne, asisti tatu na Pacome manne na asisti tatu.

Wengine waliofunga na kuasisti ni Aziz Ki bao moja na asisti moja kama ilivyo kwa Mudathir Yahya wakati Ibrahim Bacca akifunga mawili, Kennedy Musonda moja. Clatous Chama, Kibwana Shomari, Chadrack Boka na Salum Abubakar kila mmoja ana asisti moja.

Ukiangalia namna ambavyo Yanga inacheza wakati haina mpira utagundua ni timu hatari kiasi gani kutokana na namna wachezaji wanavyowalazimisha wapinzani kufanya makosa ili wao waumiliki mpira.

Katika kulazimisha wapinzani wafanye makosa pindi Yanga ikiwa haina mpira, wachezaji wa timu hiyo wanakwenda kukaba kwa kasi na kama ikikutana na timu ambayo haina uharaka wa kupanga mashambulizi, hujikuta inapoteza mpira kirahisi na kumilikiwa na Yanga ambayo inatumia pasi zisizozidi tatu kuuweka mpira nyavuni.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mbinu hiyo imewalipa mara tatu katika mechi tano za ligi. Mbili dhidi ya Dodoma Jiji ambapo mabao ya Mzize (dk 37) na Dube (dk 62) yalipatikana baada ya Yanga kukabia juu na kuchukua mpira kutokana na makosa ya wachezaji wa Dodoma Jiji huku matukio yote hayo Mudathir akihusika kutoa pasi za mwisho.

Shambulizi lililozaa bao la Mzize baada ya wapinzani kupoteza tu mpira ukatua miguuni mwa Mudathir, kwa haraka akampa Mzize akafunga kisha bao lingine la Dube wapinzani walipopoteza mpira Aziz Ki akauwahi na kuuweka kwa Mudathir, Dube akafunga. Pia katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao Yanga ilishinda 4-0, bao lililofungwa na Dube (dk 44) lilitokana na makosa ya wapinzani waliokuwa wanamiliki mpira wakapokonywa kirahisi. Hapa wapinzani walipopoteza mpira, Mzize akauwahi na kumpasia Aziz Ki ambaye alitoa asisti kwa Dube nyavu zikatikisika.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Akizungumzia anavyojenga kikosi chake, Ramovic alisema anafurahia kuona wanaimarika ingawa bado wanapaswa kuongeza uharaka uwanjani. “Soka la kisasa linahitaji zaidi kuwa na uharaka ndani ya uwanja na hiyo ndiyo tunaifanyia kazi zaidi ili kufikia malengo ya kubeba mataji mengi na kucheza nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika siku zijazo,” alisema Ramovic.

Related Posts