Mama na mwanaye wakutwa wamefariki dunia chumbani kwa kukosa hewa

Karagwe. Watu wawili, mama na mtoto wake, wamekutwa wamefariki dunia ndani ya chumba wanachoishi huku chanzo kikitajwa kuwa ni kukosa hewa baada ya kuacha jiko la mkaa likiwaka usiku wakati wamelala.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Joseph Ngonyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la katika Mtaa wa Ruzinga, kata Bugene iliyopo Wilaya ya Karagwe huku akiwataja marehemu kuwa ni Albina Staslaus (24) na mwanaye Annastazia Staslaus (6), mwanafunzi shule ya msingi Kiluluma.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Januari 30, 2025 kuhusu tukio hilo, Kamanda Ngonyani amesema jana Januari 29, 2025 saa 3 asubuhi, walipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa na mara moja askari wa jeshi hilo walifika eneo husika na kukuta watu hao wakiwa wamefia ndani ya chumba kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.

Taarifa za awali zimebaini kwamba wawili hao wamefariki kwa kukosa hewa kwani wakati wa kulala waliacha jiko likiwa linawaka.

“Askari wetu wakiwa wameambatana na daktari kutoka Kituo cha Afya cha Kayanga, Dk Kanizius Bitakwate wamefika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali na kubaini kuwa chanzo cha kifo ni kukosa hewa baada ya kuacha jiko likiwaka muda mrefu wakati wa kulala.

“Hivyo, tunatoa tahadhari kwa wananchi wote kuhakikisha wanazima majiko wakati wa kulala na kuacha tabia ya kupikia ndani,” amesema Ngonyani.

Kamanda Ngonyani amesema tangu Januari mosi hadi Januari 30, 2025, tukio hilo ni la saba kutokea katika Mkoa wa Kagera, yanayotokana na moto yakiwa sita na moja na maokozi.

Mkazi wa Mtaa wa Ruzinga ambaye ni mume wa marehemu Albina na baba mtoto Annastazia, Stadius Bernardo amesema yeye hakuwepo nyumbani wakati tukio linatokea kwa maana alikuwa kwao kitongoji cha Kiluluma, Kijiji cha Kamagambo.

Amesimulia kuwa marehemu mke wake, mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa jana saa 3 asubuhi na usiku alijaribu kumpigia simu lakini ilikuwa haipokelewi.

“Nilimpigia simu mke wangu usiku kujua hali ya nyumbani simu ilikuwa haipokelewi hadi nilipopata taarifa asubuhi ya leo kuwa mke wangu na mtoto wamefariki. Imeniuma sana maana nilikuwa nawategemea sana na mtoto wangu alikuwa wa kwanza, nilikuwa namtafutia uhamisho wa shule ya kijijini kuja huku mjini,” amesimulia Bernardo.

Daktari kutoka Kituo cha Afya cha Kayanga, Dk Kanizius Bitakwate ambaye alihusika katika uchuguzi wa mili ya marehemu hao amesema katika uchunguzi amebaini kuwa walikosa hewa safi ndiyo chanzo cha kifo.

“Baada ya kufika hapo na maaskari tumeona walikuwa wanapikia ndani na baada ya kupima miili ya marehemu nimebaini walikosa hewa safi wakiwa ndani ya chumba”amesema Dk.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Ruzinga, Stephan Simoni amesema baada ya vipimo vya daktari Jeshi la Zimamoto liliamuru miili ya marehemu ipelekwe nyumbani kwao kata ya Bushangaro kwa ajili ya maziko.

“Tumesikitika sana kufuatia wanajamii wenzetu kufia ndani ya nyumba kwa moto, uongozi wa Jeshi la Zimamoto na mtaa tumekubaliana baada ya kubaini chanzo basi marehemu wafanyiwe mazishi nyumbani kwao Bushangaro,” amesema Simon.

Hata hivyo, ameomba Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya moto hasa wananchi wenye tabia ya kujenga nyumba bila kuweka milango ya dharula.

Related Posts