Tanzania yapiga hatua kubwa kwa mujibu wa ripoti ya Absa ya viashiria vya masoko ya fedha 2024

Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya fedha kwa mujibu wa ripoti ya Absa ya viashiria vya Masoko ya Fedha – AFMI ( Absa Financial Markets Index ) 2024 iliyozinduliwa leo Jijini Dar es Salaam, ikipanda kutoka alama 50 hadi alama 52, na kujikita katika nafasi ya 12 miongoni mwa mataifa 29 yaliyotathminiwa barani Afrika.

Ikiwa katika mwaka wake wa nane, AFMI ni ripoti maarufu barani Afrika, ambayo hupima maendeleo ya sekta ya fedha katika nchi za Afrika, ikitathmini vigezo sita vikuu, ambavyo ni kuenea kwa soko, upatikanaji wa fedha za kigeni, uwazi kwenye soko na kanuni, maendeleo ya mifuko ya penseni, mazingira ya uchumi ngazi ya kitaifa, na kutekelezeka kwa makubaliano ya kifedha.

Akiongea katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya AFMI , Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi, alipongeza kundi la makampuni la Absa Group kwa kujitolea kukuza uwazi na ufanisi katika masoko ya fedha barani Africa kupitia ripoti ya AFMI. “ Mafanikio yaliyobainishwa katika ripoti hii ni ushahidi wa juhudi za ushirika miongoni mwa serikali, Benki Kuu ya Tanzania, na washirika wa soko la fedha katika kuboresha masoko hayo,” alisema.

Moja ya maeneo ambayo Tanzania imeonyesha kupiga hatua ni Upatikanaji wa Fedha za Kigeni, ikipanda kutoka alama 53 hadi alama 60, hasa kutokana na Benki Kuu ya Tanzania kuchapisha Miiko ya utendaji katika Soko la Fedha za Kigeni Miongoni mwa Mabenki ( Interbank Foreign Exchange Market code of conduct,), ikiingiza kanuni 52 kati ya 55 zinazotambuliwa kimataifa ( FX Global Code Principles).

Eneo la pili ni Uwazi katika Mazingira ya uchumi ngazi ya Kitaifa, ambapo imepanda kutoka alama 80 hadi 85, ikichagizwa na uwazi, ikiwemo umma kuruhusiwa kufahamu ratiba ya mkutano wa sera ya fedha, mfumuko mdogo wa bei, na kupungua kwa uwiano wa mikopo chefuchefu kwenye makampuni ya biashara.

Eneo la tatu ni uwezo wa soko la fedha kufikia watu wengi zaidi, ambapo maendeleoa katika nyanja hii yanatokana na kutolewa kwa dhamana ya makampuni (corporate bonds) zenye thamani ya Dola za Marekani 300m, na kuziduliwa kwa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo zinazorandana na maadili ya Dini ya Kiislamu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser, alisisitiza umuhimu wa ripoti ya AFMI katika kuchochea kukua kwa masoko ya fedha barani Afrika. “ Kupanua masoko ya fedha na vilevile kuyafanya yafikie watu wengi zaidi ni muhimu kwa hatua inayofuata ya maendeleo barani Afrika,” alisema mkurugenzi huyo. “ Tunayo fahari kushirikiana na OMFIF katika kutayarisha ripoti hii, ambayo inafanya kazi kama dira miongoni mwa watunga sera na wawekezaji.

Tukio la uzinduzi wa ripoti ripoti hiyo inayoheshimika ilihudhuriwa na wadau, watunga sera, na watalaam wa masuala fedha, ambapo walipata fursa ya kubadilishana mawazo huku wakitathmini taarifa hiyo na jinsi gani inahusiana na utendaji wa masoko ya fedha nchini Tanzania.

Uzinduzi huo vilevile ulihudhuriwa na maofisa wakuu wa Absa Group, ambao walichangia uzoefu wao kwenye maendeleo yanayojitokeza kwenye sekta ya fedha ambayo yanaamua muundo wa masoko ya fedha Afrika, ikiwemo teknolojia za kidijitali, na juhudi za kuboresha vyombo vya sheria na vinavyosimamia kanuni.

Ripoti hiyo, inayotayarishwa kwa kushirikiana na OMFIF, inatoa taarifa muhimu kwa wawekezaji wa watunga sera, huku ibainisha fursa kwa upande moja, na vilevile maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho kwenye masoko ya fedha barani Afrika.

Wajkati huohuo, ripoti hiyo imebanisha maneo mawili ambayo Tanzania inapaswa kuyafanyia maboresho, ikiwemo mifuko ya pensheni, ambapo ripoti imedokeza haja ya kuimarishwa kwa uwezo wa kuwekeza wa wadau wa ndani. Na vilevile uboreshaji wa mfumo wa sheria ili kuinua kiwango cha imani ya miongoni wawekezaji.

Richard Magongo, Mkurugenzi wa Bodi – Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi na Mazingira Hatarishi, kwa niaba ya Paul Makanza, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Benki ya Absa Tanzania, pamoja na kuwashukuru waliohudhuria hafla hiyo, alisisitiza haja ya kufanyia maboresho ya maeneo nchini Tanzania yalioainishwa kwenye ripoti.

“ Pamoja na kuwa kuna maendeleo yamepatikana, bado kuna kazi ya kufanya hasa kwenye maeneo kama mifuko ya pensheni na mifumo wa kisheria,” alisema Magongo. “ Absa inaahidi kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha masoko ya fedha nchini Tanzania yanaendelea kukua.”

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Bot), Bw. Emmanuel Tutuba ( wa tatu kushoto) akikata utepe wakati akizindua ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2024, jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Masoko ya Kifedha wa Absa Afrika, Bw. Anthony Kirui, Mkurugenzi wa Masoko ya Kifedha wa Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira, Mkurugenzi wa Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser, mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Absa kutoka Ofisi ya Kanda, Bw. Jeff Gable na Mjumbe wa Bodi wa benki hiyo, Bw. Richard Magongo.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Bot), Bw. Emmanuel Tutuba ( wa tatu kushoto) akipokea tuzo ya shukrani kutoka kwa Mkurugenzi wa Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser baada ya uzinduzi wa ripoti ya Absa ya Viashiria vya Masoko ya Fedha Afrika 2024, jijini Dar es Salaam Leo. Kutoka kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela,Mkurugenzi wa Masoko ya Kifedha wa Absa Tanzania, Bi. Irene Rwegalulira, Jeff Gable kutoka Absa Afrika na Mjumbe wa Bodi wa benki hiyo, Richard Magongo.

Related Posts