ALIYEKUWA kocha wa Yanga raia wa Argentina, Miguel Gamondi amekubali kujiunga na timu ya Al Nasr ya Libya baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi miwili, tangu alipoachana rasmi na kikosi hicho cha Jangwani, Novemba 15, mwaka jana.
Taarifa kutoka Libya zinadai kocha huyo aliyeipa Yanga mafanikio zaidi amesaini mkataba wa miezi sita hadi mwishoni mwa msimu huu, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, ikiwa kikosi hicho kitafanya vizuri kwenye michezo yao.
Gamondi aliondoka Yanga, Novemba 15 mwaka jana na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Saed Ramovic, baada ya kuiongoza timu hiyo msimu huu katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara, ambapo kati yake alishinda minane na kupoteza miwili pamoja na minne ya raundi ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika alipoivusha kutinga makundi.
Hatua ya Gamondi kufukuzwa ilijiri baada ya Yanga kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu akianza na kipigo cha 1-0 kutoka Azam Novemba 2 kisha kugongwa 3-1 na Tabora United Novemba 7, mwaka jana huku akiiacha timu nafasi ya pili na pointi 24.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia Nasreddine Nabi aliyeipa mataji mawili ya Ligi Kuu, mawili ya Kombe la Shirikisho (ASFC), mawili ya Ngao ya Jamii na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Tangu ateuliwe, Gamondi alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo alishinda 34, sare miwili tu na kupoteza minne. Katika michezo hiyo 40 ya msimu uliopita na huu wa sasa, safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho cha Gamondi ilifunga jumla ya mabao 85 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, ambapo kiujumla kwa misimu yote miwili alikusanya pointi zake 104.
Gamondi amechukua mataji matatu na timu hiyo akianza na Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kuifanya Yanga kufikisha jumla ya mataji 30, tangu mwaka 1965, akachukua pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii mwaka 2024.
Pia, aliipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024 baada ya miaka 25 tangu iliposhiriki mara ya kwanza 1998 ikiwa chini ya Tito Mwaluvanda kabla ya kuachiwa Raoul Shungu na kurudia tena msimu huu kabla ya kufurushwa kumpisha Ramovic.