Kocha Msauzi amvaa Fadlu | Mwanaspoti

SIMBA inarudi uwanjani wikiendi hii ikiwa ugenini ili kutaka kulinda hadhi iliyonayo ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara itakapoikabili Tabora United, lakini kule katika michuano ya kimataifa kuna kocha mmoja Msauzi ameamua kuitumia salamu mapema kabla droo ya hatua ya robo fainali haijafanyika.

Simba ni kati ya timu nane zilizopenya robo baada ya kuongoza Kundi A, ikifuatiwa na CS Constantine ya Algeria, hivyo kuwa na nafasi ya kukutana na timu tatu zilizomaliza nafasi ya pili katika makundi ya B, C na D ambazo ni Asec Mimosas ya Ivory Coast, Al Masry ya Misri na Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Nyingine zilizopenya hatua hiyo ni watetezi Zamalek ya Misri, RS Berkane ya Morocco na USM Alger ya Alger ambazo zilikuwa vinara wa makundi matatu yaliyosalia ya B, C na D, ambao hawawezi kukutana na Mnyama kama ilivyokuwa kwa Constantine waliokuwa nao kundi moja.

Kabla droo ya mechi za hatua hiyo hazijapangwa, kocha wa Stellenbosch, Steve Barker ameliambia Mwanaspoti kwamba anafahamu timu hiyo inaweza kukutana na Simba robo-fainali lakini wala hana presha endapo wataangukia kwa wekundu hao, kwani tayari ameshazisoma karibu timu zote.

Hata hivyo, Barker alisema endapo watakutana na Simba hautakuwa mchezo rahisi kutokana na uzoefu wa wekundu hao huku akimtaja kocha mkuu wa Msimbazi, Fadlu Davids kuwa ni kocha mzuri ambaye anapenda soka la kushambulia.

Barker alisema, ili Stellenbosch iwe salama katika hatua hiyo wanatakiwa kuwa na hesabu bora kwa kuhakikisha wanashinda vizuri nyumbani kabla ya kwenda ugenini kwa kuwa wekundu hao wana rekodi bora wanapokuwa Kwa Mkapa.

“Hatuwezi kuwa na hofu, huu ni mchezo wa soka kama tukikutana na Simba ni wazi itakuwa mechi ngumu kwetu na hata kwao, hizi ni timu mbili zinazocheza soka kama linalofanana, kocha wao (Simba)  Fadlu Davids tunajuana vizuri  ni kocha mzuri,” alisema Barker na kuongeza;

“Katika kundi letu tulikutana na timu ngumu sana kama RS Berkane, nadhani tumepata changamoto nzuri na kwenye mechi kama hizi kama kweli tutaanzia nyumbani tunatakiwa kutengeneza matokeo mazuri, ukiiangalia Simba unaona namna walivyo wazuri wakiwa nyumbani zaidi ya ugenini kama mkifanya makosa ya kuwaruhusu wafanye maamuzi.”

Simba katika mechi tatu za makundi imeshinda mechi tatu nyumbani, huku ugenini ikipoteza moja, ikishinda moja na kutoa sare moja.

Stellebosch ikiwa nyumbani ikishinda mbili kati ya tatu, huku ugenini ikishinda moja na kupoteza mbili.

Pia Barker akizungumzia ubora wa Simba alisema timu hiyo ina uimara mkubwa katika eneo la kiungo zaidi huku akiitaja safu yao ya ulinzi inaweza kufanya makosa endapo itapewa presha.

“Nilikuwa naziangalia timu zote ambazo tutakutana nazo, angalia Simba wako vizuri sana kwenye eneo la kiungo ukikutana nao unatakiwa kuwanyima utulivu lakini wanafanya makosa pia hasa eneo la ulinzi hivyo kila kitu kinawezekana.”

Katika misimu saba mfululizo ambayo Simba imeshiriki michuano ya CAF tangu iliporudi upya msimu wa 2018-2019, timu hiyo imetinga robo fainali mara sita, ikiwamo nne za Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili za Kombe la Shirikisho, japo haikuwahi kutinga nusu kitu kinachosubiriwa kwa msimu huu.

Related Posts