Pamba Jiji yapata CEO, aachiwa kufyeka mishahara

KLABU ya Pamba Jiji imemtambulisha, Peter Rehett kuwa ofisa mtendaji mkuu (CEO), ikiwa ni takriban miezi 10 nafasi hiyo ikiwa haina mtu ikikaimiwa na meneja wa timu hiyo, Ezekiel Ntibikeha.

Rehett ambaye ni mkuu wa Idara ya Tehama katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza na mara nyingi amekuwa akikaimu nafasi ya mkurugenzi wa halmashauri ya jiji hilo, ametambulishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda wakati wa chakula cha usiku na wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na wadau wa timu hiyo.

Akimtambulisha CEO huyo, RC Mtanda amesema pamoja na sababu za kiufundi kuchangia timu hiyo kufanya vibaya, lakini ukosefu wa uongozi imara ni miongoni mwa sababu za kuyumba na kusababisha iwe kama  kambale ambao kila mmoja anajiona ana ndefu na hamheshimu mwingine.

Mtanda ambaye ni mlezi na mshauri wa Pamba Jiji amesema sababu kubwa za kumteua Rehett ni kutokana na ukorofi na misimamo yake, hivyo wamempa mamlaka ya kuisimamia na kuiendesha timu hiyo ikiwemo kutimua viongozi au wachezaji wasiofuata sheria na kanuni.

Mamlaka nyingine ni kukata Sh100,000 kwa siku kwa wachezaji wanaochelewa mazoezini na kupendekeza watu walioshindikana ili waondolewe moja kwa moja klabuni, huku akitakiwa kutokuwa na huruma au kucheka na yeyote.

“Huyu (CEO) yuko pale halmashauri mnaofanya kazi pale mnamjua tabia zake ni zipi. Ni mkorofi lakini ukorofi wa kusimamia ukweli na taratibu, tumesema kwenye timu kama Pamba ambapo kuna watu ni kama jeshi la kambale wana masharubu marefu wanatakiwa wapewe mtu kama huyu,” amesema Mtanda.

“Na wewe (CEO) tumekuambia kalia kiti inavyotakiwa wala usimuulize Kibamba (Kiomoni – mkurugenzi wa Jiji) wala mkuu wa Mkoa, ukiona kuna mtu hafuati utaratibu na sheria wewe kanuni unazo zitumie. Na tukakubaliana mchezaji akichelewa mazoezi atakatwa Sh100,000 kwa siku.”

Mtanda amemtaka mtendaji huyo kuhakikisha kila mchezaji anapewa na kusaini miiko na taratibu za kazi zikiwemo zinazokataza uvutaji bangi na kuchelewa mazoezini ili kuhakikisha hawajengi timu mbovu isiyo na nidhamu.

“Sheria unazo katiba unayo endesha timu tumekukabidhi wewe na kama kuna mtumishi wa Pamba Jiji ana utovu wa nidhamu mchukulie hatua kali, na ukisema huyu nimemshindwa mlete kwetu tunamtoa siku hiyo hiyo maana hii timu ilikuwa haijulikani mkubwa nani mdogo nani inakuwa jeshi la kambale aliyezaliwa leo ndevu jana ndevu.”

Mwenyekiti wa timu hiyo, Bhiku Kotecha amesema usajili mkubwa walioufanya dirisha dogo utawapa matokeo mazuri, huku akisisitiza kuwa mwenyekiti wa bodi na baraza la madiwani wamebariki shughuli zote zinazoendelea wanachohitaji ni ushindi wa timu yao.

Related Posts