Kifahamu kidonge cha aspirin ndogo na matumizi yake

Tangu uhuru mpaka mwishoni miaka ya 1990, dawa iliyokuwa ikijulikana sana katika huduma za afya kutumika kukabiliana na maumivu na homa ilikuwa ni aspirin.

Kwa hivi sasa wagonjwa wenye umri kati ya miaka 40-70 ambao wanahudhuria kliniki za moyo ni kawaida kujiuliza ni kwa nini wanapewa aspirini hiyo, lakini yenye jina la junior aspirin.

Ukweli ni kuwa dawa hii kongwe duniani moja ya matumizi yake muhimu ni kinga tiba katika kiwango kidogo kwa baadhi ya wagonjwa walio katika hatari ya kupata shambulizi la moyo, kitabibu heart attack.

Aspirin ndogo ipo katika kiwango cha chini kitabibu, hujulikana kama junior au baby aspirin. Daktari anaweza kupendekeza kutumia kila siku ikiwa umewahi kupata kiharusi au shambulizi la moyo.

Au, ikiwa uko katika hatari kubwa ya shambulizi la moyo, ikiwamo waliofanyiwa upasuaji wa moyo au waliopata maumivu ya kifua yaliyotokana na ukosefu wa oksjeni katika misuli ya moyo, kitabibu hujulikana angina.

Kifamasia aspirini inajulikana kama salicylate, ni dawa isiyo ya steroidal ya kuzuia shambulizi la mlipuko wa kinga ya mwili (NSAID).

Inafanya kazi kwa kuzuia vitu vinavyotiririshwa mwilini na kinga ya mwili baada ya kupata uchokozi ili kupunguza maumivu na uvimbe.

Haishauriwi kumpa mtoto wa chini ya miaka 12, na ni muhimu sana kuiweka mbali na watoto hii kwa sababu katika kiwango kikubwa ni sumu kwa mwili.

Pia katika kiwango cha chini cha aspirini ndogo hutolewa kwa baadhi ya wagonjwa kuzuia damu kuganda. Hii hupunguza hatari ya kupata kiharusi na mshtuko wa moyo.

Iwapo hivi karibuni ulifanyiwa upasuaji kwenye mishipa iliyoziba, daktari anaweza kukuelekeza utumie aspirini kwa kiwango cha chini ili kuzuia kuganda kwa damu kwa kuzuia chembe sahani zisishikane. Ikiwa unatumia dawa ili kujitibu, fuata maelekezo yote kwenye kifurushi cha bidhaa au zingatia maelekezo ya daktari au mfamasia. Ikiwa una maswali yoyote usisite kuwauliza.

Tembe za aspirini ndogo huweza kutafunwa vizuri kabla ya kumezwa. Ikiwa tumbo litauma unapotumia dawa hii, unaweza kuinywa pamoja na chakula au maziwa.

Kipimo na urefu wa matibabu hutegemea hali yako na mwitikio wa matibabu. Soma lebo ya bidhaa ili kupata mapendekezo kuhusu vidonge vingi unavyoweza kutumia katika kipindi cha saa 24 na muda ambao unaweza kujitibu kabla ya kutafuta ushauri wa matibabu.

Usichukue dawa zaidi au usichukue kwa muda mrefu kuliko ilivyopendekezwa, isipokuwa kama umeelekezwa na daktari wako.

Habari nzuri kuhusu aspirini ndogo ni kuwa kiasi kilichomo humo kina madhara machache ukilinganisha na aspirini kubwa.

Aspirini inaweza kusababisha vidonda kwenye utumbo, hasa ukiitumia kwa muda mrefu au kwa dozi kubwa.

Pia inaweza kusababisha kuvuja kwa damu kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo.

Kushikamana na ushauri wa madaktari kunaepusha kukutana na madhara machache yasiyohitajika. Faida ya kutumia dawa hii ni kubwa kuliko madhara machache yanayotokea.

Related Posts