Dodoma. Serikali imesema ndugu wa marehemu ndiyo chanzo cha baadhi ya miili ya wapendwa wao kubaki hospitalini kwa kisingizo cha kuzuiliwa, lakini si madaktari.
Kauli ya Serikali imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel kuwa katika ufuatiliaji wa kuchukua hatua, Serikali imebaini kuwa kuzuiliwa kwa maiti si tatizo la madaktari bali la ndugu.
Dk Mollel ametoa kauli hiyo bungeni leo Januari 31, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea (CCM), Bonnah Kamoli ambaye amehoji ni hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia maiti kutokana na deni la matibabu, kinyume na maelekezo ya Serikali.
“Maiti huwa zinazuiliwa na uongozi wa hospitali zetu na wala si suala la madaktari na katika maeneo ambayo tumefanya ufuatiliaji ili kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi husika, tumebaini ndugu wa marehemu ndio waliokataa kufuata utaratibu uliowekwa, ili kuzuia hoja za ukaguzi,” amesema Dk Mollel.
Naibu Waziri amesema ndugu hao wakishindwa kufuata utaratibu huanza kulalamika na kukimbilia kwenye vyombo vya habari na kwa viongozi, wakiwemo kwa wabunge.
Amesema Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Na. 1 wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.
Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kufuata utaratibu na wabunge waendelee kutoa elimu ili kusaidia kuzuia hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Licha ya maelekezo ya kila maa ya Serikali, tatizo la kuzuiliwa maiti hospitali limekuwa likijirudia katika maeneo mbalimbali nchini.
Januari 20, 2024, aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alizitaka hospitali zote za umma kutekeleza kwa ukamilifu maelekezo yaliyokwisha tolewa na Serikali ya kutozuia miili ya marehemu kwa kigezo cha kushindwa kulipa gharama za matibabu.
Ummy alitoa agizo hilo akijibu swali la aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Paul Makonda katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tanga.
Makonda aliuliza ni upi mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wananchi maskini wanaoshindwa kulipia gharama za matibabu kwa kudaiwa kulipia maiti, ilhali hawana uwezo wa kilipa deni na kukomboa mwili.
“Naomba nitumie mkutano huu kuzitaka hospitali zote za serikali, marufuku kuzuia maiti ya Mtanzania yeyote, haya ndiyo maelekezo ya Serikali, nawataka waganga wafawidhi wa hospitali zote za Serikali nchini kuzingatia mwongozo wa Serikali wa kutozuia maiti, tafuteni njia nyingine, toeni maiti wakizika mtakuja kudaiana mambo mengine,” alisema Ummy.