Mangalo ndo basi tena hadi msimu ujao!

BEKI wa zamani wa Biashara United na Singida Foutain Gate, Abdulmajid Mangalo amesema licha ya kuwa nje ya uwanja, lakini anatumia muda huu kuwafuatilia wachezaji kujifunza vitu kwa ajili kurejea msimu ujao.

Mangalo aliyekuwa tegemeo katika kikosi cha Singida Fountain Gate kwa sasa yuko nje ya uwanja akiendelea kuuguza jeraha la goti na matarajio yake ni kurudi kibaruani msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mangalo amesema licha ya ofa alizopokea katika dirisha dogo, lakini ameamua kupumzika kujiweka fiti zaidi ili msimu ujao anaporudi uwanjani awe imara.

Mchezaji huyo amesema wakati huu akiendelea na mazoezi binafsi chini ya uangalizi wa wataalamu, anaendelea kufuatilia waliomzidi ili kujifunza vitu akieleza kuwa kiwango chake hakitabadilika.

“Kwa sasa afya inaimarika na nilipata ofa kadhaa dirisha dogo ila niliamua kuendelea kujiimarisha kwanza ili msimu ujao nijue naanzia wapi, naendelea kujifua wapo watalaamu wananisimamia,” amesema Mangalo.

“Sijakaa tu naendelea kufanya mazoezi binafsi kwakuwa mpira ndio kazi yangu lakini nafuatilia waliopo uwanjani ili niweze kupata kitu, kukaa nje msimu mzima siyo kitu kidogo.” 

Ameongeza kuwa kwa kuwa hadi sasa yupo huru kukipiga popote, hatakuwa na masharti magumu kwa timu itakayohitaji huduma yake akieleza kuwa mipango yake ni kuona anacheza soka.

“Niwashukuru wadau wanaoendelea kufuatilia afya yangu na kunisapoti. Kwa sasa niko huru na nitakuwa tayari kucheza popote, kimsingi ni makubaliano na pande zote,” amesema nyota huyo aliyewahi kuhusishwa pia na timu za Simba na Yanga kwa vipindi tofauti licha ya dili hizo kutotiki.

Related Posts