KIUNGO mshambuliaji wa Kagera Sugar, Peter Lwasa amesema anatamani mzunguko wa pili wa Ligi Kuu afunge mabao matano na kufikisha 10 msimu huu.
Nyota huyo raia wa Uganda alisajiliwa na Kagera Sugar msimu huu akitokea KCCA ya nchini kwao alikodumu msimu mmoja.
Tanzania inakuwa nchi ya nne kucheza soka baada ya Uganda (KCCA na URA), Kenya (Sofapaka, Kariobangi Sharks na Gor Mahia) pamoja na DRC Congo alikoitumikia Lubumbashi Sports.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lwasa amesema anatamani duru la pili afunge mabao matano ili kufikisha 10 ambayo anaamini yatamfanya awe na msimu bora wa kwanza akiwa Tanzania.
“Sitaki kujipa presha raundi hii, lakini natamani kufunga mabao hayo ambayo kwangu itakuwa mwanzo mzuri wa ligi ya Tanzania ambayo ina ushindani mkubwa,” amesema.
“Ligi ya Bara sasa hivi inafuatiliwa sana huko nje, lengo langu ni kupambana na kupanda hata kucheza ligi kubwa Afrika.”
Kesho, Kagera Sugar itakuwa ugenini katika Uwanja wa KMC Complex kucheza dhidi ya Yanga na hapa Lwasa anaeleza maandalizi ya mchezo huo.
“Ni mchezo mgumu, wapinzani wetu wamebadilika tofauti na tulivyokutana mwanzo. Mchezo uliopita tulipoteza, lakini tulicheza vizuri. Safari hii tutapambana angalau kupata pointi, ongezeko la wachezaji wapya pia limeongeza ushindani,” amesema mchezaji huyo.
Kiungo huyo ndiye anayeongoza kwa wafungaji Kagera Sugara akiwa na mabao matano.