Trump atoa kauli mgogoro wa Rwanda, DR Congo

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump amesema mgogoro kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) “ni tatizo kubwa sana.”

Trump amebainisha hilo Alhamis Januari 30, 2025 akijibu swali la mwandishi aliyemuuliza kuhusu kinachoendelea baina ya Rwanda na DRC, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ajali ya ndege iliyotokea Washington.

“Unaniuliza swali kuhusu Rwanda, ni tatizo kubwa sana, nakubali, lakini sidhani kama inafaa kwa sasa kulizungumzia. Lakini ni tatizo kubwa sana,” amesema Trump.

Mgogoro kati ya Rwanda na DRC ni mzozo wa muda mrefu unaohusisha masuala ya kisiasa, kiusalama, na kijamii.

Migogoro hii imechochewa na historia ya vita, makundi ya waasi, na mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa waasi ambaye wapiganaji wake wameiteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameapa kuendelea na mashambulizi hadi mji mkuu, Kinshasa.

Corneille Nangaa, ambaye anaongoza muungano wa makundi ya waasi ambayo yanajumuisha M23, amenukuliwa akisema lengo lao kuu ni kupindua Serikali ya Rais Félix Tshisekedi.

Taarifa za vyombo vya habari ambazo hazijathibitishwa zinasema waasi hao kwa sasa wanasonga mbele kuelekea Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano

Katika hotuba ya televisheni baada ya kuanguka kwa Goma, Rais Tshisekedi alisema “mwitikio wa nguvu na ulioratibiwa” ulikuwa unaendelea ili kutwaa tena eneo hilo kutoka kwa waasi.

“Tunawahakikishia jambo moja: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haitaruhusu kufedheheshwa au kupondwa. Tutapigana na tutashinda,” alisema Jumatano jioni.

Mapigano hayo yamewalazimu takribani watu 500,000 kuondoka kwenye makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu, kwa mujibu wa UN.

Jana Alhamisi, Nangaa aliwatambulisha waasi hao kama wasimamizi wapya wa Goma, akiwaambia waandishi wa habari kwamba ndio wamekita mizizi katika eneo hilo.

Tangu mapigano yalipoongezeka wiki iliyopita, umeme ulikatika na usambazaji wa maji ukiwa wa shinda na chakula kikiwa kichache, imeripoti BBC.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts