Dar es Salaam. Kiongozi wa kundi la Kiislamu la Hayat Tahrir al-Sham (HTS), Ahmed al-Sharaa ameteuliwa kuwa Rais wa mpito ya Syria, ikiwa ni takriban siku 53 zimepita tangu alipoongoza kuondolewa madarakani uongozi wa Bashar al-Assad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Januari 30, 2025 na Kamanda Hassan Abdel Ghani, msemaji wa Kamandi ya Operesheni za Kijeshi nchini Syria, Ahmad al-Sharaa atakuwa Rais wa mpito na ameidhinishwa kuunda baraza la muda la kutunga sheria.
“Tunatangaza kuteuliwa kwa Kamanda Ahmad al-Sharaa kuwa mkuu wa nchi katika kipindi cha mpito. Atachukua madaraka ya rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Syria na kuwakilisha nchi katika majukwaa ya kimataifa,” imesema taarifa hiyo.
“Rais ameidhinishwa kuunda baraza la kutunga sheria la muda kwa awamu ya mpito, ambalo litafanya kazi zake hadi katiba ya kudumu itakapotungwa na kuanza kutumika.”
Al-Sharaa ndiye aliyeongoza mapinduzi ya kumng’oa madarakani Rais Bashar al-Assad mnamo Desemba 8, 2024. Kufuatia kuondoka kwa Assad, al-Sharaa amechukua nafasi ya uongozi katika serikali ya mpito ya Syria.
Kiongozi huyo katika agizo lake la kwanza, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha makundi yenye silaha nchini humo akitaka silaha zote, zikiwemo zile zinazoshikiliwa na vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi, kuwekwa chini ya mamlaka ya Serikali.
“Hatutaruhusu kabisa kuwepo na silaha nchini nje ya udhibiti wa Serikali, iwe kutoka kwa makundi ya wanamapinduzi au makundi yaliyopo katika eneo la SDF,” amesema.
Al-Sharaa pia ametoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa wakati wa utawala wa Assad, akisema hatua hizo zinaadhibu watu wa Syria badala ya uongozi wa zamani.
Ameomba msaada wa kimataifa katika kushtaki uhalifu uliofanywa na utawala wa Assad na kurejesha mali zilizoibwa kutoka kwa Wasyria.
Pia ameeleza nia ya kuepusha mzozo na Israel, akieleza kuwa Syria haitatumika kulenga nchi nyingine na kusisitiza haja ya masuluhisho ya kidiplomasia ili kuhakikisha usalama.
Vilevile ameahidi kulinda madhehebu yote madogo ndani ya Syria, kutetea kuishi pamoja na umoja. Amekiri hitaji la kujenga upya taasisi za Serikali na kuandaa katiba mpya, mchakato anaotarajia utachukua muda.
Endelea kufuatilia Mwananchi.