Dodoma. Mpango wa utekelezaji wa azimio la kuwa na sarafu moja ifikapo 2024 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, umesogezwa mbele kwa miaka saba mingine na sasa mpango huo unatarajiwa kufikiwa 2031.
Katika swali lake bungeni leo Januari 31, 2025, Mbunge wa Kinondoni (CCM) Abbas Tarimba ameuliza utekelezaji wa azimio la kuwa na sarafu moja ifikapo 2024 katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umefikia hatua gani?
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Denis Londo ametoa sababu za kuahirishwa kwa mpango huo licha ya kwamba Tanzania ilishakuwa tayari baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa.
Naibu Waziri ametaja vigezo hivyo ni kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kisichozidi asilimia 8; kiwango cha juu cha nakisi ya bajeti kisichozidi asilimia 3 ya pato la Taifa; kiwango cha juu cha deni la Taifa kisichozidi asilimia 50 ya pato la Taifa husika; na akiba ya fedha za kigeni ya kutosheleza mahitaji kwa miezi minne na nusu.
“Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo; athari za Uviko – 19 na uhaba wa miundombinu muhimu, nchi wanachama zimeshindwa kufikia malengo ya kuwa na sarafu moja katika mwaka uliopita 2024,” amesema Naibu Waziri.
Amesema kutokana na tathmini hii, mpangokazi wa awali umehuishwa na muda wa utekelezaji umeongezwa hadi ifikapo mwaka 2031, na mpango kazi mpya umetoa msisitizo kwa nchi kutekeleza kikamilifu hatua za awali wa mtangamano, kufikia vigezo vilivyokubalika.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, tathmini ya mwaka 2022 ilionyesha kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki bado zilikuwa hazijatekeleza kikamilifu hatua za awali za mtangamano, baada ya nchi nyingi kushindwa kufikia vigezo vya kuoanisha uchumi mpana.
Awali, Naibu Londo amesema kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi Wanachama zilikubaliana kutekeleza mpango wa miaka 10 (2014-2024) ili kufikia azma ya kuwa Umoja wa Fedha na Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2024.
Katika kipindi cha miaka 10 kabla ya kufikia Umoja wa Fedha na Sarafu Moja, nchi za Jumuiya zilitakiwa kutekeleza kikamilifu hatua za awali za mtangamano, ambazo ni ushirikiano katika Soko la pamoja na Umoja wa Forodha na kuanzisha taasisi muhimu za kusimamia utekelezaji.