Mwanza. Wadau wa michezo nchini, ndugu, jamaa na marafiki wameuaga mwili wa Mkurugenzi wa Kituo cha Michezo na shule za Alliance, James Bwire na kesho Jumamosi Februari mosi, 2025 utasafirishwa kwenda kwao Nyamwaga, Tarime kwa maziko yatakayofanyika Jumapili.
Bwire ambaye enzi za uhai wake alikuwa mdau wa michezo nchini kupitia kituo cha kukuza na kulea vipaji cha Alliance, amezalisha wachezaji wanaotamba ndani na nje ya nchi.
Alifariki Januari 25, 2025, saa 4 usiku wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Waombolezaji hao wameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almasi Kasongo.
Akizungumza kwenye kusanyiko hilo, Kidao amesema sekta ya michezo nchini imepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa mhimili mkubwa katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Amesema kituo cha Alliance kimezalisha wachezaji wengi ambao ni tegemeo kwa timu za taifa na wengine wanacheza nje ya nchi ambako baadhi ya ada za uhamisho wao, zinapaswa kuinufaisha Alliance, hivyo, watafanya mazungumzo na familia ya Bwire ili ipata fedha hizo.
“Sisi TFF tumeguswa na huu msiba, Alliance kilikuwa ni kituo chetu cha kimkakati, vijana wengi wametoka hapa tumefanya vitu vikubwa chini ya Alliance. TFF tutahakikisha tunaendeleza na maono ya Bwire ili yadumu,” amesema Kidao na kuongeza:
“Hata ndoto za vijana wenye vipaji vinatimizwa bila changamoto zozote, kwa hiyo tutakaa na wanafamilia na tutaongea kwa sababu kuna fedha ambazo zinatokana na vijana wanaocheza Ulaya, ambao wamelelewa hapa, tutakaa kuona familia inanufaika nazo vipi.”
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Bwire atakumbukwa kwa mambo muhimu matatu ambayo ni mwanamichezo aliyetoa heshima kwa mkoa huo kwa kuhakikisha unapata timu ya Ligi Kuu, alikuwa jemedari wa kuongoza mapambano ya kitaaluma ili kuinua maendeleo ya elimu, na alikuwa kiongozi shupavu.
Mtanda ameiomba jamii kuiunga mkono familia ya mkurugenzi huyo kwa kuendeleza ndoto alizoziishi na kutamani kuzitimiza ili kuhakikisha shule za Alliance zinaendelea na hazipotezi mwelekeo.
“Nilimfahamu Bwire miezi michache iliyopita, alikuja ofisini mara mbili lakini tulionana mara moja, akaniomba nimsaidie timu ya wasichana (Alliance Girls) isishuke daraja, akasema ‘nina imani ukiingiza nguvu yako kidogo timu hii haitashuka daraja’,” amesema Mtanda.
Ameongeza kuwa: “Walikuwa wamebakiza mechi tatu dhidi ya Yanga Princess, Baobab Queens na Ceassia Queens, kwa hiyo nilifanya kazi ambayo yeye alinitaka nifanye na Alliance Girls haikushuka daraja.”
Mwakilishi wa umoja wa vijana waliosoma Alliance, Jimmyson Masinga amesema: “Ametufundisha kufanya kazi kwa juhudi ili kuleta maendeleo kwa taifa na alitulea katika misingi ya usawa.
“Alikuwa anaweza kuamka saa 10 usiku kuja kutukagua mabwenini, kwa hiyo alifanya shule kuwa kama sehemu ya familia yake.”
Mmoja wa wanasiasa, Charles Chinchibela wa Chadema amesema alimshinda Bwire kwenye uchaguzi wa nafasi ya diwani, kata ya Mahina mwaka 2010 lakini hakukata tamaa na mwaka 2015 aligombea tena na kushinda.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema wilaya hiyo imempoteza mdau mkubwa wa maendeleo na mwekezaji katika sekta ya elimu na maendeleo.
Bwire (56) alizaliwa Desemba 7, 1969 katika Kijiji cha Kisangola, Kata ya Nyamwaga Wilaya ya Tarime mkoani Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto tisa wa familia ya Bwire Manga.
Alianza kusumbuliwa na maradhi ya moyo mwaka 2016, ameacha watoto saba, wanne wa kiume na watatu wa kike na wajukuu wawili.