Malasusa: TRA kusanyeni kodi kwa uaminifu kuondoa shaka

Dar es Salaam. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasisitiza watumishi wake wakusanya kodi kiuaminifu li walipa kodi wasiwe na mashaka juu ya fedha zinazokusanywa.

Hiyo amesema itasaidia kuongeza ari ya watu kulipa kodi na kuondoa ukwepaji kodi ambao umekuwa ukilalamikiwa na TRA mara zote.

Dk Malasusa ameyasema hayo leo Januari 31 wakati akizungumza na ujumbe wa TRA uliomtembelea ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa mahusiano bora kati ya Mamlaka hiyo na taasisi mbalimbali.

“Tukiona maendeleo tunajua ni sababu ya kodi za Watanzania, ndiyo zinatupeleka mbali na tunakuwa na maisha bora. Kama kanisa lingetamani tuwe na kasi ya maendeleo nchini ili kuwafanya Watanzania ambao hawajapata fursa ya kulipa kodi walipe, sababu inakusanywa vyema na wanaopaswa kutoa wanatoa, wakusanyaji wanakusanya kiuaminifu,” amesema Askofu Malasusa.

Amesema kodi ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi na hakuna muujiza katika hilo.

“Shida iliyopo wanaolipa ni wachache lakini kwa juhudi zinazoonekana, tunaona nuru inayokuja kuwa wanaohusika kulipa kodi watalipa, makusanyo yatakuwa mengi na wanaokatwa hawatakuwa na maumivu kwa sababu ni wengi wanaotoa,” amesema Dk Malasusa.

Kinachoonekana sasa ni wengi kutoelewa athari hasi za kutolipa kodi na kuwa suala hilo kuwa ni sawa na kumfanya mwanadamu asiwe na damu.

Tutatoa elimu na kuwakumbusha waumini kutoa na kulipa kodi. Maandiko yako wazi kwamba sisi tunatakiwa kuheshimu mamlaka na kuwezesha, kwani kodi haijaanza leo, ipo na hakuna nchi inayoendelea bika kukusanya kodi

Akizungumzia suala hili, Kamishna wa TRA, Yusuph Mwenda amesema waumini wa KKKT ni miongoni mwa walipa kodi na TRA iko tayari kufanya nao kazi ili kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari ndani ya nchi.

“TRA ni taasisi ya Watanzania, tumepewa kazi ya kukusanya kodi kwa ajili ya masilahi ya Watanzania wote, hivyo tunaweza kushirikiana kutoa elimu ya kodi, tuko tayari kushirikiana kwa kuangalia namna ya kutoa elimu ili mlipakodi ajue kodi anayopaswa kulipa kwa wakati gani na wapi, hii ni elimu ya kodi ambayo tupo tayari kuitoa,” amesema Mwenda.

Ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi, Mwenda amesema imewekwa mifumo rahisi utakayowezesha mtu kulipia kodi sehemu yoyote atakayokuwepo.

“Ili kiwapo na usawa wa kulipa kodi lazima wote walipe lakini kuna wachache wanakwepa kwa kutokutoa risiti, kutoa risiti bandia, mwingine hajauza chochote anatoa risiti ili apate faida ya kodi, kuwa na stempu bandia katika vinywaji au kuleta magendo,” amesema Mwenda

Related Posts