WANASEMA jaMBO likimalizika, basi hufuata au lilelile huendelea na hivyo kuwafanya watu kuendelea kulifuatilia au kuanza upya kufuatilia linalojitokeza.
Hivyo ndivyo ilivyo pia kwa supastaa wa Yanga, Maxi Mpia Nzengeli ambaye pale Jangwani ni kama ameanza kutengeneza ufalme flani ndani ya kikosi cha Jangwani, licha ya kwamba hatajwi sana.
Basi ndoto za klabu ya Simba kutaka kumsajili kiungo huyo mshambuliaji mahiri ni kama zimekwama, baada ya bosi mkubwa aliyemuibua nyota huyo kuamua kuwachomolea ombi lao na kuamua kumbakisha rasmi Jangwani.
Mapema wiki hii, Mwanaspoti lilinasa taarifa mabosi wa Simba walikuwa wakipiga hesabu kali za kimafia kwa kutaka kumsajili Maxi kwa kuamua kupiga simu moja kwa moja kwa mmiliki wa mchezaji huyo, Jenerali Amissi Kumba ili kuulizia mkataba alionao Jangwani, japo inajua ulikuwa ukingoni.
Hata hivyo, wakati Simba ikisubiri majibu tu, maamuzi ya mwisho yamefanyika baada ya bosi mkubwa wa AS Union Maniema inayommiliki Maxi, kumaliza kila kitu akiwaambia wasaidizi wake ndani ya klabu hiyo, hatma ya kiungo huyo kuondoka Yanga labda itokane na kushindwana na timu hiyo.
Maniema inayomilikiwa na Jenerali Kumba ndiye aliyetoa msimamo huo akisema, Yanga ni klabu rafiki na kufanya mazungumzo ya kumweka sokoni Maxi ni kama kuwakosea.
“Jenerali amezuia mazungumzo hayo ya Simba kuhusu Maxi kama ni mchezaji mwingine ni sawa, lakini sio Maxi, unajua kuna kitu Yanga walifanya kwetu Maniema, msimu huu unakumbuka tulikuja hapo Tanzania, kujiandaa na msimu mpya na tukakaa katika kambi yao na gharama kubwa walilipa wao viongozi wa Yanga kile kitu Jenerali anaona ni kitu kikubwa sana tulifanyiwa kina thamani sana,” alisema bosi huyo na kuongeza.
“Hatua hiyo imemfanya Jenerali atuambie Yanga wasipewe presha yoyote juu ya Maxi kwanza ni mchezaji wao, watamalizana naye kwa kuwa hata Yanga wenyewe wamesema Maxi atasaini mkataba mpya wakati wowote kuanzia sasa.”
Wakati Maniema wakijibu hivyo, Rais wa Yanga Injinia Hersi Said akiwa Morocco katika mkutano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), amekutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Maniema, Guy Kilongozi na klabu hizo mbili zikakubaliana kila kitu juu ya uhakika wa Yanga kubaki na kiungo huyo.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic mara alipotua Jangwani akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi alionekana kuvutiwa na Maxi kwa namna anavyopambana ndani ya uwanja akisema ni mchezaji anayekimbia eneo kubwa la uwanja kisha kuwaambia mabosi anataka abaki naye.
Maxi ambaye huu ndio msimu wa pili na wa mwisho kimkataba, hatua ambayo imewavutia Simba kuanza umafia wa chinichini kusaka saini yake, ndiyo kwanza amerejea uwanjani kutoka majeruhi yaliyomweka nje kwa muda akikosa baadhi ya mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara.