UHONDO wa Ligi ya Championship unaingia mzunguko wa 17, wikiendi hii na baada ya jana kuchezwa michezo mitatu kwenye viwanja tofauti, leo itapigwa mingine mitatu kuwania pointi tatu.
Mchezo wa mapema utapigwa saa 8:00 mchana kwenye kituo cha michezo cha TFF Tanga na African Sports iliyoichapa mabao 2-1, Cosmopolitan mechi ya mwisho, itawakaribisha Maafande wa Green Warriors waliochapwa pia 2-1 na Mtibwa Sugar.
Saa 10:00 jioni itapigwa michezo miwili na Bigman FC iliyoichapa Mbeya City bao 1-0, mechi ya mwisho itaendelea kusalia kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi kuikaribisha Songea United, yenye kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-1 na Mbeya Kwanza.
Mchezo wa mwisho leo, utapigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita na wenyeji Geita Gold iliyokumbana na kichapo cha mabao 2-1, dhidi ya TMA ya jijini Arusha, itaikaribisha Mbuni FC iliyowafunga Maafande wa Polisi Tanzania mabao 2-0.
Kesho Jumapili utapigwa mchezo mmoja na Kiluvya United iliyochapwa mabao 3-1 na Stand United, itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani kujiuliza mbele ya Biashara United iliyotoka kuwafunga Maafande wa Transit Camp bao 1-0.
Raundi ya 17, itahitimishwa keshokutwa Jumatatu na Transit Camp itasalia kwenye Uwanja wa Mabatini kuikaribisha Stand United inayoingia katika mechi hiyo na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Kiluvya United kwa mabao 3-1.
Kocha wa Stand United, Juma Masoud alisema licha ya kujiunga na kikosi hicho kwa kipindi cha muda mfupi ila atahakikisha anaendelea kukipambania kutoshuka ndani ya nne bora, huku akisifu pia kiwango cha wachezaji wanachoendelea kukionyesha.
“Nashuruku nimepokelewa vizuri na kwa muda niliokuwa nao wamekuwa wepesi wa kupokea na kufanyia kazi maelekezo ambayo nimekuwa nikiyatoa, raundi ya pili ni ngumu kwa sababu ushindani unakuwa ni mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu.”