Dar es Salaam. Hatimaye majina 1,520 ya wafanyabiashara walio na sifa na vigezo vya kurejea katika Soko Kuu la Kariakoo yamewekwa hadharani.
Sanjari na hilo, wafanyabiashara zaidi ya 366, hawataruhusiwa kurudi sokoni hapo hadi watakapolipa madeni waliokuwa wanadaiwa na Shirika la Masoko kabla soko halijaungua.
Hatua hii inakuja baada ya kukamilika kwa ukarabati na ujenzi wa ghorofa ulioanza baada ya soko kuungua Julai 10, 2021, ambapo na serikali ilitoa Sh29 bilioni ili lifanyiwe ukarabati ambao ulienda sanjari na ujenzi mpya wa soko dogo.
Jana Ijumaa Januari 31, 2025 taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na Ofisa Uhusiano Mkuu wa shirika hilo, Revocutus Kasimba, ilisema orodha ya majina hayo ya watakaorejeshwa yatapatikana kwenye tovuti ya <Shirika www.kariakoomarketcolz> na iIe ya Ofisi ya Rais-Tamisemi <www.tarnisemi go.tz>
Hata hivyo, Kasimba amesisitiza wale wafanyabiashara 366 wanaodaiwa na Shirika zaidi ya Sh358 watapaswa kulipa deni hilo kabla hawajapatiwa nafasi za biashara.
Kabla ya hatua hii, mchakato wa kutoa majina ya waliopitishwa kurejea kwenye uhakiki ulikwama Julai 2024 baada ya orodha ya awali kugomewa na wafanyabiashara kwa kile walichodai viongozi wao hawakushirikishwa.
Hata hivyo, ili kufikisha kilio chao hicho Julai 12, 2024 walikusanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja kisha kuandamana hadi ofisi ndogo za Chama cha Mapinduzi, Lumumba jijini hapa.
Julai 13,2024 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alikutana nao na kuridhika na hoja zao, ambapo pamoja na mambo mengine aliamuru majina 819 yaliyokuwa yamepitishwa yaondolewe kwenye mfumo na kufanyika uhakiki upya.
Januari 30, 2025 Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Hawa Ghasia, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa uhakiki huo umeshakamilika na orodha mpya ingetolewa wiki hii.