Tani 400,000 za korosho zauzwa kupitia stakabadhi ghalani

Dodoma. Wakulima wa korosho wamepata Sh1.4 trilioni baada ya kuuza tani 408,687.7 katika mfumo wa stakabadhi ghalani katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 31, 2025, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa usimamizi wa ghala kupitia CCTV wa Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) pamoja na stika ya utambuzi wa ghala.

Amesema kwa mauzo hayo imewezesha Serikali kukusanya Sh42.9 bilioni. Amesema katika zao la Ufuta jumla ya tani 144,619.7 zimeuzwa kupitia mfumo huu ambapo wakulima wamepata Sh520.6 bilioni na Serikali imepata Sh15.6 bilioni.

Katika upande wa mbaazi, Dk Jafo amesema tani 99,682.9 zimeuzwa kupitia mfumo huo, wakulima wakipata Sh199.4 bilioni na Serikali imepata Sh6.0 bilioni.

Kuhusu faida za mfumo wa kidijitali, waziri huyo amesema mfumo huo utaimarisha usalama wa bidhaa, kuhakikisha uwazi na uwajibikaji, kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara.

Amesema pia manufaa kwa kampuni za bima pamoja maanufaa kwa taasisi za kifedha (mabenki na wakopeshaji wanaotumia stakabadhi za ghala kama dhamana).

Kaimu Mkurugenzi wa WRRB, Asangye Bangu amesema kupitia mfumo huo, wataweza kufuatilia maghala yote yaliyosajiliwa chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani wakiwa mkoani Dodoma.

Hata hivyo, amesema licha ya kuwa na mfumo huo ambao utawawezesha kuona na kufuatilia uendeshaji wa magahala, watakwenda kuona, kuchukua hatua kwa mambo ambayo watayaona kupitia mfumo huo.

Bangu amesema mfumo wa stakabadhi ghalani unatekelezwa katika mikoa yote isipokuwa mikoa mitatu ya Arusha, Iringa na Njombe.

Naye mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya WRRB, Alex Domitius amesema wamepata changamoto ya upotevu wa magunia 365 yenye thamani ya Sh406 katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.

“Bodi yangu kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya ilichukua hatua kuhakikisha tunamwajibisha ipasavyo kisheria mtunza ghala yule (hakumtaja) na kuwajibika kufidia hasara hiyo,” amesema.

Amesema hadi leo amelipa Sh391 milioni na kuwa wanamdai Sh15 milioni.

Akiwawakilisha waendesha maghala, Mkurugenzi wa Kampuni ya Cropstan Investiment Ltd, Simon Nkana amesema asilimia kubwa ya mazao yanayotunzwa ghalani huwa yana unyevu.

“Sasa katika haya mazao unavyotoa na kupokea kuna kiwango cha unyevu kinashuka ambacho huondoka na uzito wa zao husika. Wadau wenzetu wameshindwa kulitambua hili kuwa ikitokea unyaufu maana yake uzito unapungua na hivyo uzito unaoingia na zao si unavyotoka,” amesema.

Amesema suala hilo, limewapa jina baya waendesha maghala na baadhi wameitwa kuwa ni wezi lakini anaamini kuwa kuna jambo la kisayansi na kuomba Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kufanya utafiti na kuja na kiwango cha mazao baada ya kutunzwa ghalani.

Naye Mkuu wa Chuo Cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga amesema wako katika hatua ya kusaini makubaliano na bodi hiyo ili kushirikiana nao kwenye kutoa elimu itakayowajengea uwezo waendesha maghala pamoja na wamiliki.

“Ili sasa leseni (za uendeshaji wa maghala) ziwe zinatolewa wakiwa wameshapata utaalamu. Huko tunakokwenda tutawafikia waendesha maghala wote nchini,” amesema.

Related Posts