Mwanza. Wakati Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza ikitoa taarifa ya kuokoa fedha zaidi ya Sh366.9 milioni zilizokuwa hatarini kupigwa, wataalam wameshauri mbinu kudhibiti mianya ya upotevu wa makusanyo ya Serikali.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Takukuru kati ya Oktoba hadi Desemba 2024, Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Idrisa Kisaka amesema fedha hizo zimedhibitiwa kupigwa katika eneo la ukusanyaji kodi ya zuio ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwenye mnada wa mifugo wa Misungwi mkoani humo.
Kisaka amesema bila kuffanya ufuatiliaji wa mwenendo wa ukusanyaji wa mapato katika maeneo hayo fedha hizo zingekuwa hatarini kutoingizwa katika akaunti za mapato za Serikali.
“Tumefanikisha kuzuia upotevu wa fedha hizo kupitia uchambuzi wa mfumo, ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, uelimishaji umma, uchunguzi na utekelezaji wa programu ya Takukuru rafiki, ambayo inatoa fursa kwa raia kutoa taarifa wanapobaini mianya ya rushwa,” amesema Kisaka.
Katika hatua nyingine, Kisaka amesema Takukuru katika kipindi hicho, imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 13 yenye thamani ya zaidi ya Sh4.4 bilioni ambapo miradi 12 kati yake yenye thamani ya zaidi ya Sh3.9 bilioni ilikutwa na upungufu.
“Baada ya kubaini upungufu huo tuliwataka na kuwashauri kuyafanyia marekebisho ili kuleta ubora, sambamba na kuleta thamani halisi ya fedha iliyotumika,” amesema.
Amesema baada ya ufuatiliaji, Takukuru imebaini upungufu ulioainishwa umefanyiwa kazi na watekelezaji wa miradi hiyo katika sekta ya elimu, barabara na biashara kwa zaidi ya asilimia 65 jambo linaloifanya kuwa na kiwango kilichokusudiwa.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Msingi Mabuki wilayani Misungwi mkoani humo unaogharimu Sh351 milioni, ujenzi wa Sekondari ya Bugoro wilayani Sengerema (Sh584 milioni) na ujenzi wa barabara ya Bupandwa hadi Kusekeseke wilayani Sengerema kwa kiwango cha changarawe (Sh414 milioni).
Pia kuna mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Kilabela wilayani Ilemela mkoani humo (Sh584 milioni), Sekondari ya Maseleme (Sh584 milioni), na mradi wa ujenzi wa nyumba vya madarasa, jengo la utawala kwa mfumo wa ghorofa na matundu ya vyoo wilayani Nyamagana mkoani humo (Sh561 milioni).
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na upotevu wa mapato ya Serikali, Mchambuzi wa Masuala ya Biashara na Fedha, Dk Ntui Ponsian ameiomba Serikali kujikita kwenye uwekezaji wa mifumo na vifaa.
Dk Ntui ambaye ni mhadhiri katika Idara ya Uhasibu na Fedha ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT) Mwanza amesema endapo TRA ingekuwa inafanya kazi kwa kuzingatia mifumo na kutumia vifaa ipasavyo ikiwemo mashine za EFD, Takukuru wasingekuwa na kazi ya kuchunguza ama kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
“Bila uwepo wa mifumo thabiti na vifaa vya kutosha kwenye maeneo ya biashara na kwenye minada bado hata Takukuru haitoweza kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali kwa asilimia 100. Si ajabu hata hizo walizookoa ni asilimia isiyofika hata 20 ya fedha zilizopotea,” amesema Dk Ponsian.
Dk Ponsian amesema endapo Serikali itawekeza fedha kwenye uimarishaji wa mifumo ya ukusanyaji mapato na mashine, mamlaka ikiwemo TRA na Takukuru zitapunguziwa kazi hatimaye kutumia rasilimali watu iliyopo kufanya shughuli zinazosuasua ikiwemo utoaji wa elimu ya rushwa na kodi kwa Umma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) taifa, Shaban Itutu amesema rushwa katika jamii haitotokomezwa endapo jamii haitokuwa na hofu ya kufanya alichokiita ‘wizi’ wa fedha za umma.
Itutu ameshauri maeneo yenye vitega uchumi vya Serikali kufungwe kamera za usalama ili kurahisisha ufuatiliaji wa watendaji wa Serikali wanaochepusha mapato na kusaidia kupata vielelezo na ushahidi wa matendo yao.
“Tumekuwa tukishuhudia Takukuru kila siku wanasema wamemkamata mtu fulani kwa tuhuma za rushwa, watampeleka mahakamani lakini baadaye utashangaa yuko mtaani kwa sababu labda kaachiwa kwa kukosekana ushahidi ila tukiwa na kamera ushahidi unakuwepo,” amesema Itutu.
Kwa upande wake, Mkazi wa Nyamadoke wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Sylvia Juma ameiomba Takukuru kuendelea kufukua na kukagua utekelezaji na usimamizi wa miradi ya umma ili kuiepushia Serikali hasara inayotokana na uchepushaji wa mapato hayo.