HAMAS, wamethitibisha habari ya kuuawa kwa makamanda wake kadhaa katika mashambulizi ya Israel kwenye eneo lililozingirwa kila upande la Ghaza.
Makamanda kadhaa wameuawa akiwemo mkuu wake wa majeshi, Mohammed Deif. Mkuu wa Brigedi za al-Qassam, Abu Obeida alithibitisha kuuawa kamanda huyo pia Naibu Kamanda wa kijeshi wa HAMAS, Marwan Issa katika mapigano na Israel.
Makamanda wengine waliouawa katika vita hiyo ni pamoja na Ghazi Abu Tama’a, kamanda wa silaha na huduma za kivita, Raed Thabet, kamanda wa wafanyakazi na mkuu wa kitengo cha vifaa na Rafeh Salama, kamanda wa Brigedi ya Khan Younis.
Wengine waliouawa ni Kamanda Mohammed Deif Ahmed al-Ghandour, kamanda wa Brigedi ya Kaskazini na Ayman Nofal, kamanda wa Brigedi ya katikatika mwa Ghaza, waliuawa katika mapambano hayo na Israel.
Mohammad ‘Abu Khaled’ Deif, aliyekuwa maarufu kwa kutoonekana kirahisi, aliwahi kunusurika kuuawa katika majaribio saba wakati wa uhai wake katika mapambano na utawala wa Israel. Alikuwa mtu muhimu katika kuandaa operesheni za kijeshi dhidi ya Israel.
Vyombo vya habari vilitangaza habari ya kuuawa kwa kamanda Deif, lakini tangazo la juzi la Abu Obeida ni uthibitisho wa kwanza rasmi kutoka kwa Hamas juu ya kuuawa kwa makamnda wao hao.