RC Serukamba azionya taasisi zisizotumia mfumo wa NeST

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital-Iringa

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ametoa onyo kwa watendaji wa taasisi nunuzi wanaotumia visingizio mbalimbali kukwepa kutumia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) unaosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Serukamba ametoa onyo hilo Mei 13, 2024 mjini Iringa wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya Mfumo wa NeST kwa Wakurugenzi wa Bodi na Menejimenti ya PPRA.

Amesema matumizi ya mfumo huo unaosimamiwa na PPRA ukiwa umeunganishwa na mifumo kumi na saba (17) ya Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi, kupunguza muda na gharama za michakato ya ununuzi, kudhibiti vitendo vya udanganyifu, rushwa na kuzuia ukosefu wa maadili, yamethibitisha nia ya dhati ya Serikali ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha kwenye ununuzi wa umma.

Ameongeza kuwa pamoja na jitihada hizo, wapo baadhi ya watendaji wa taasisi nunuzi wenye sababu zao binafsi wanaweka visingizio mbalimbali ili wasitumie Mfumo wa NeST kwakuwa wanafahamu unawabana kufanya ubadhirifu.

Amesema kufanya hivyo ni kukiuka maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Nichukue nafasi hii sasa, kuweka msisitizo kwa kuzitaka taasisi zote za umma katika mkoa huu kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha kila ununuzi wanaoufanya unapitia kwenye Mfumo wa NeST.

“Natambua, wapo baadhi ya watendaji wa taasisi nunuzi wenye sababu zao binafsi wanaweka visingizio mbalimbali ili mradi tu wasitumie Mfumo wa NeST kwakuwa wanafahamu unawabana kufanya ubadhirifu. Nitoe onyo kwa watendaji wenye tabia hii isiyofaa na kuwasihi wawe wazalendo,” amesema Serukamba na kuongeza kuwa:

“Mkoa wa Iringa umeyapokea maelekezo ya Serikali ya kuwa kila ununuzi wa umma lazima ufanyike kupitia Mfumo wa NeST pekee. Na mimi kama kiongozi wa mkoa huu ninalo jukumu la kuhakikisha maelekezo ya Mheshimiwa Rais yanatekelezwa na hivyo hili nitalisimamia kikamilifu,” amesema.

Sehemu ya washiriki.

Aidha, Serukamba ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mageuzi makubwa kwenye kila sekta nchini ikiwemo sekta ya ununuzi wa umma kwa kuwezesha ujenzi wa mifumo inayodhibiti ubadhirifu na kuongeza ufanisi katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Amesisitiza kwamba mageuzi hayo yamesaidia kuongeza ufanisi hususani kwenye kusimamia ununuzi wa umma kwa kuhakakisha Serikali inapata thamani ya fedha kwenye kila miradi na huduma zinazotolewa.

“Napenda kuipongeza PPRA kwa usimamizi wenye tija na bora wa sekta ya ununuzi wa umma, nimefurahi kusikia kuwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuwa mifumo isomane imetekelezwa vizuri kwenye huu Mfumo wa NeST, kwani nimeambiwa kuwa mifumo 17 imeunganishwa kwenye mfumo huu na kwamba bado mifumo mingine inaendelea kuunganishwa,” amesema Serukamba.

mesisitiza kuwa matumizi ya mfumo huu yamethibitisha nia ya dhati ya serikali ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali fedha kwenye ununuzi wa umma ambao unakadiriwa kutumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali.

“Sisi sote ni mashahidi kwamba matumizi ya mfumo huu yameleta tija kubwa yameziba mianya ya rushwa, yameongeza uwazi na uwajibikaji, na yote haya ni katika kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha,” ameeleza.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA, Dk. Leonada R. Mwagike, alisema sambamba na mafanikio ambayo Mamlaka hiyo imeyapata bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya taasisi nunuzi kutoheshimu maagizo ya Rais ya kutumia mfumo wa NeST kwa sababu zao binafsi.

Amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi muhimu ya utawala bora ikiwemo kuzielekeza taasisi nunuzi kufanya ununuzi kwa kuzingatia weledi, uadilifu, uzalendo, uwazi, usawa na kuheshimu miiko ya utumishi wa umma.

Related Posts