WAANDAJI wa Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2025 wametangaza kuongeza muda wa washiriki kuchukua nambari zao za ushiriki pamoja na T-shirts za ushiriki, zoezi linalotarajiwa kuanza katika kipindi cha wiki mbili zijazo Jijini Dar es Salaam.
Zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi baada ya kufungwa kwa zoezi la kujiandilisha ili kushiriki mbio hizo kukamilika, ambapo idadi iliyokuwa imewekwa ya washiriki katika mbio za kilomita 42 na zile za kilomita 21 tayari zimejaa hata kabla ya Februari 6, mwaka huu, tarehe ambayo ilikuwa imewekwa kama siku ya kufunga zoezi la kujiandikisha kushiriki.
“Tumeongeza muda wa kukusanya nambari hizo na T-shirts hadi nyakati za jioni ili wale wanaotoka kazini nyakati hizo waweze kuchukua nambari zao Jijini Dar es Salaam na Arusha ili kupunguza msongamano wa dakika za mwisho mjini Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji, zoezi la ukusanyaji wa nambari hizo utaanza rasmi Ijumaa Februari 14, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City Mall (mbele ya Samaki Samaki) kuanzia saa 10 alasiri hadi saa moja za jioni ambapo siku ya Jumamosi Februari 15 na Jumapili Februari 16, zoezi hilo litaanza saa nne (4) asubuhi hadi saa 12 za jioni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, zoezi hilo litahamia Jijini Arusha Jumanne ya Februari 18 na Jumatano Februari 19, ambapo ukusanyaji wa nambari hizo utafanyika katika hoteli ya Kibo Palace kuanzia saa kuanzia saa 8 mchana hadi za moja ya jioni.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa sehemu ya mwisho ya ukusanyaji wa nambari itakuwa ni mjini Moshi siku ya Alhamisi Februari 20 kuanzia saa 6 za mchana hadi saa 11 jioni, Ijumaa Februari 21 kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 12 za jioni na Jumamosi Februari 22 kuanzia saa 4 asubuhi hadi s11 jioni, zoezi ambalo litafanyikia uwanja wa michwezo wa chuo kikuu cha Uhsirika Moshi (MoCU).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya waandaaji, nambari za Mbio za kilomita 5 zinazofadhiliwa na benki ya CRDB bado zinaendelea kuuzwa ambapo wanaotarajiwa kushiriki wanaweza kujiandikisha kupitia Mixx by YAS (zamani Tigopesa) kwa kupiga *150*01#, kisha kubonyeza 5 LKS, kisha kubonyeza 6 (Tiketi) na kufuata maelekezo ili kukamilisha usajili wao au mtandaoni kupitia www.kilimanjaromarathon.com. Aidha wanaotarajia kushiriki wamekumbushwa ya kuwa kuna idadi ndogo katika mbio hizo pia na tayari asilimia 60 ya nafasi hizo tayari zimeshachukuliwa.
Aidha waandaaji hao wamewataka washiriki hao kuzingatia nyakati zilizotangazwa ili kuepuka usumbufu na pia wametoa wito kwa wale wanaokusanya nambari kwa ajili ya marafiki au ndugu zao kuhakikisha wanakuwa na nakala za vitambulisho vya wanaowachukulia pamoja na barua za ridhaa zinazowaruhusu wawakilishi wao kuchukua kwa niaba yao
Pia imewaonya wale wanaotarajia kukimbia na nambari zisizo rasmi (nambari feki) ambapo wale watakaobainika kufanya hivyo wataondolewa kwenye orodha ya ushiriki na kufungiwa kushiriki mbio Kilimanjaro International Marathon.
Waandaaji hao pia walisema kuwa mbio hizo ni tukio muhimu na kwamba wandaaji hawatavumilia wale watakaokiuka kwa njia moja au nyingine kanuni za mbio hizo ikiwemo ya kufanya jambo lolote lile ambalo litaweza kuathiri au kuleta mgongano wa kimaslahi kwa wadhamini wa mbio hizo ambao ni Kilimanjaro Premium Lager Marathon, Yas Kili Half Marathon na CRDB Bank Fun Run.
Wadhamini wa mwaka huu ni pamoja na wadhamini wakuu Kilimanjaro Premium Lager ambao wanadhamini mbio za kilomita 42, wadhamini wa kilomita 21 YAS, wadhamini wa mbio za kujifurahisha za kilomita 5 benki ya CRDB Bank, pamoja na wadhamini wengine wa meza za maji ni Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies na TPC Sugar, pamoja na washirika rasmi-GardaWorld Security, CMC Motors, Hoteli za Salinero –Kilimanjaro na wasambazaji rasmi Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Kili Marathon huandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions Limited.