Katika kuhakikisha zoezi la usafi linakua la kudumu, Mkuu wa wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka wananchi, wafanyabiashara na taasisi zote ndani ya halmashauri hiyo kufanya usafi kuwa zoezi la kudumu.
Mkuu huyo wa wilaya ya Ilala ameyazungumza hayo wakati wa zoezi maalum la usafi lililofanyika february mosi 2025.
Mpogolo amesema mkakati wa Ilala ni kwa Kanda namba 1 na 2 za Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kuanzia eneo la Kamata, Mtaa wa Gerezani kupitia barabara ya Sokoine, Kivukoni front, Luthuli, barabara ya Barack Obama kuelekea fukwe za Dengue kufanyike usafi wa kila mara.
Amesema ili zoezi ilo liwe endelevu kwa kila mwananchi, taasisi, wafanyabiashara na wadau wengine waweke utaratibu wa usafi kila siku kabla na baada ya kuanza na kumaliza shughuli zao wahakikishe mazingira yanakua safi.
Mpogolo amebainisha viongozi wamekubaliana kulifanya Jiji la Ilala kuendeleza usafi wa mazingira, taasisi, makazi na fukwe zote kuendelea kuwa safi.
Mpogolo amesisitiza zoezi la usafi kwa sasa katika wilaya ya Ilala ni la kila siku, huku zoezi la usafi wa pamoja la kila mwisho wa mwezi litaendelea ikiwa ni pamoja na kampeni za usafi za kila mara kuweka jiji safi.
Aidha Mpogolo ametoa wito kwa Wananchi, Taasisi na wadau mbalimbali wa mazingira kujitokeza katika mazoezi ya usafi endelevu ili kuhakikisha jiji la Ilala linaendelea kuwa safi kwa jitihada za pamoja kutokomeza uchafu na magonjwa ya mlipuko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam amesema ofisi yake itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufanyia usafi vinapatikana katika mazoezi hayo kwa kushirikiana na Wakandarasi wa usafi wanaofanya kazi ndani ya jiji la Ilala.